JUMIKITA YAIPONGEZA SERIKALI KWA KUIMARISHA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI, WAZIRI MKUU ATAJA MIKAKATI

 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka mamlaka zinazohusika na usimamizi wa sekta ya habari na wadau wengine kuandaa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo viongozi na wanachama wa Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandaoni ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA) ili waendelee kuripoti habari zao kwa maslahi ya umma.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumanne, Mei 21, 2024 katika Kongamano la Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandaoni ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA) kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa habari za mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ili kuhakikisha kuwa sekta hiyo inaendelea kukua na kuchangia kuleta maendeleo kwa Taifa.

“Kupitia vyombo vya habari, hasa vya mitandao ya kijamii, tumeweza kuwahabarisha wananchi kuhusu shughuli na mipango ya Serikali, na kuhamasisha ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli na mipango hiyo.”  
 
Ameongeza kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha Sheria na Miongozo inayosimamia sekta ya habari ili kuweka mazingira wezeshi kwa wanahabari kufanya kazi zao kwa uhuru na kwa kuzingatia maadili, tamaduni na haki za watu wengine.
 
 
“Katika kipindi hiki cha miaka mitatu toka Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani amewezesha kukua kwa sekta ya habari na hasa ongezeko la watumiaji na  wasomaji wa habari kupitia mitandao ya simu.”
 
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Mawasiliano wa Taifa ili kuhakikisha wadau katika ngazi zote wanapata taarifa za kutosha na wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi na kuimarisha mawasiliano ya Serikali.

Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameilekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iandae utaratibu wa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa waandishi wa habari za mitandaoni ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili na utamaduni wa Kitanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JUMIKITA, Shaban Matwebe ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyosimamia ukuaji endelevu wa sekta ya habari nchini ikiwemo kuimarisha uhuru wa vyombo hivyo.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa akizungumza kwenye kongamano hilo.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akizungumza kwenye kongamano hilo.



Mwenyekiti wa JUMIKITA, Shaban Matwebe akizungumza kwenye kongamano hilo.




























Previous Post Next Post