Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, ameendelea kuwasisitiza Watanzania kuwa na hofu ya Mungu, ili kuhakikisha wanadumisha hali ya amani.
Akizungumza katika Misa ya mkesha wa Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa la Moyo safi wa Maria Parokia ya Shinyanga mjini, amesema amani ya kweli inapatikana kwa watu walio na hofu ya Mungu ndani ya mioyo yao.
Askofu Sangu pia amepongeza hatua ya Serikali ya mkoa wa Shinyanga ya kuzuia Disko Toto kama njia muhimu ya kuwalinda watoto, ambapo ametumia nafasi hiyo kuwataka wazazi na walezi kutowaruhusu watoto wao kwenda katika nyumba za starehe ili kuwaepusha na mambo mabaya ambayo wanaweza kufanyiwa, na badala yake washerehekee sikuu ya Krismasi ndani ya familia.
Amewaasa Wakristo wote kuhakikisha wanasherekea sikuu ya Krismasi kwa amani na utulivu, bila kufanya matendo maovu ambayo ni kinyume na malengo ya maadhimisho ya sikukuu hiyo, ya kuzaliwa kwa mkombozi wao Yesu Kristo.
Akiwa katika kanisa kuu la Ngokolo leo Jumapili kwa ajili ya maadhimisho ya Misa ya Krismasi, Askofu Sangu ameendelea kuwasisitiza wakristo wote kuungana kupinga vitendo vya utoaji wa mimba na ukatili kwa wanawake na watoto, huku akiwataka wale wanaotumia shida za wengine kama fursa ya kujinufaisha kuacha kufanya hivyo kwa kuwa ni chukizo mble za mwenyezi Mungu.