ASKOFU SANGU ASIKITISHWA NA KIFO CHA PAPA BENEDICT WA XVI

Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, ameeleza kupokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Baba Mtakatifu mstaafu Benidict XVI , ambacho kimetokea asubuhi ya leo .

Askofu Sangu amebanisha kuwa, amefanya kazi kwa karibu na hayati Benedict wa XVI kabla ya kung’atuka madarakani kwa zaidi ya miaka mitano, wakati yeye (Askofu sangu) akiwa afisa katika Idara ya uinjilishaji wa mataifa huko VATICAN.

Askofu Sangu amemwelezea hayati Papa Benedict kuwa alikuwa ni mtulivu, muadilifu na aliyelijua vizuri Kanisa, na alikuwa na uwezo wa kuhimili changamoto mbalimbali kutokana na moyo wake wa imani.

Daima katika utume wake kwa Kanisa, aliongozwa na kaulimbiu ya ubinadamu na utakatifu, hata pale changamoto mbalimbali zinapotokea.

Amesema Papa Benedict alijaliwa na mwenyezi Mungu kuwa na akili nyingi, ambazo amezitumia kuleta mchango mkubwa katika utume wa Kanisa kupitia utalaam wake wa masuala ya Teolojia, na ameandika vitabu vingi ambavyo vinatumiwa na Kanisa mpaka sasa.

Askofu Sangu ameahidi kuelekeza sala zake katika mumwombea, ili Mungu ampokee katika makazi yake ya Milele, ambayo aliyatumainia katika maisha yake ya hapa duniani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Vatican, Papa Benedict amefariki dunia leo tarehe 31 Desemba 2022 , saa 3: 45 Asubuhi, akiwa na umri wa miaka 95.

Amefariki dunia akiwa katika makazi yake kwenye Hosteli ya Mater Ecclesiae iliyoko kwenye Bustani za Vatican, ambako amekuwa akiishi tangu mwaka 2013 alipong’atuka madarakani.

Inaelezwa kuwa alifanya maamuzi hayo magumu, ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine, aweze kulitumikia Kanisa la Kristo Yesu, kwa ari na moyo mkuu na kwa uchungu na majonzi makuu.

Kufutia kifo hicho cha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedict wa XVI, Kanisa linawaalika watu wote kuungana na Mama Kanisa kwa ajili ya kumwombea maisha ya uzima wa milele.

Taarifa zaidi kuhusu taratibu za mazishi zitatolewa hao baadaye.

Hayati Papa Benedikto XVI  alizaliwa Aprili 16 mwaka 1927 huko Ujerumani, ambapo baada ya majiundo yake ya Kikasisi alipewa Daraja takatifu la Upadre mnamo Juni 29 mwaka 1951.

Baada ya kupata shahada ya uzamivu katika Teolojia alifundisha kwa miaka kadhaa, na kushiriki kama mtaalam katika Mtaguso mkuu wa pili wa Vatcan.

Aliteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Munchen na Frisngen nchini Ujerumani, mnamo Machi 24 mwaka 1977 na Baba mtakatifu Paul VI na akawekwa wakfu Mei 28 mwaka 1977.

Papa Paul wa VI alimteua kuwa Kardinali mnamo Juni 27 mwaka 1977, na akashiriki uchaguzi wa Baba Mtakatifu Yohane Paul II mwaka 1978.

Tarehe 25 Novemba 1981 Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, alimteua kuwa mkuu wa idara ya mafundisho ya imani na kuacha madaraka ya Jimbo mnamo tarehe 15 Februari  1982, na akashika kazi hiyo mpya mpaka alipochaguliwa kuwa Papa mwaka 2005.

Katika kutekeleza kazi hiyo, aliandaa  Katekisimu ya Kanisa Katoliki (tangu 1986 hadi 1992) na ufupisho makini  wa Katekisimu hiyo (tangu 2003 hadi 2005).

Baada ya kuchaguliwa kuwa Papa, aliendeleza juhudi za mtangulizi wake Papa Yohane Paul II, katika utekelezaji wa Mtaguso pamoja na kupambana na makwazo ya kijinsia ambapo baada ya kung’atuka kwake, alishika maisha ya sala kwa ajili yake binafsi. Kanisa na watu wote. 

Previous Post Next Post