ASKOFU SANGU KUPOKEA MAANDAMANO YENYE UJUMBE MAALUM WA KUPINGA UKATILI KWA WATOTO

 


Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, kesho Jumatano tarehe 28.12.2022, atapokea maandamano yaliyobeba ujumbe maalum wa kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Watoto watakatifu wafiadini, ambayo huadhimishwa na Kanisa kila ifikapo Disemba 28 ya kila mwaka , kwa lengo la kukumbuka watoto waliouawa kwa amri ya Mfalme Herode, siku chache baada ya kuzaliwa kwa mtoto Yesu .

Maandamano hayo ambayo yatawashirikisha watoto kutoka katika Parokia zote za Jimbo, yataanza saa 2:00 asubuhi kutoka katika Kanisa la Moyo safi wa Maria Parokia ya Shinyanga mjini na kuishia katika Kanisa kuu la Mama Mwenye Huruma la Ngokolo, na baadaye yatafuatiwa na adhimisho la Misa takatifu itakayoanza saa 4:00 asubuhi.

Kupitia maadhimisho hayo, Askofu Sangu atapata nafasi ya kuzungumza na kula chakula pamoja na watoto hao,  kama sehemu ya kuenzi mchango wa watoto katika historia ya ukombozi na utume wa Kanisa.

Kupitia maadhimisho hayo,  Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga limeona ni fursa muhimu ya kupaza sauti kupinga vitendo vya ukatili ambavyo wamekuwa wakifanyiwa watoto bila hatia, kama ilivyokuwa kwa mfalme Herode ambaye alitoa amri ya kuuawa kwa watoto wote wa kiume wa kuanzia umri wa miaka  miwili, kama njia ya kulinda ufalme wake wa Yudea kwa kuaamini kuwa, huenda mtoto Yesu aliyetajwa kuwa mfalme na wataalam wa nyota (Mamajusi) kutoka Mashariki, angemnyang’anya ufalme wake.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema kuwa “ SIMAMA IMARA MUUMINI KATIKA MALEZI BORA YA MTOTO”

Previous Post Next Post