DKT. MPANGO VIONGOZI WA SERIKALI WANACHANGIA KWA KIASI KIKUBWA UHARIBIFU WA MAZINGIRA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akifungua Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi, Mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji linalofanyika kwenye ukumbi wa Masiti Gangilonga Mkoani Iringa Leo Disemba 19,2022.

PICHA NA JOHN BUKUKU-IRINGA

……………………..

Na Fredy Mgunda, Iringa.

Baadhi ya viongozi wa serikali wanachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mazingira na vyanzo vya maji kwa ajili ya maslahi yao binafsi

Akizungumza kwenye kongamano la wahariri na wadau wa uhifadhi, mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdori Mpango akiwa Iringa leo Desemba 19,2022 amesema kuwa viongozi mbalimbali ndio wamekuwa waharibifu wakubwa wa vyanzo vya maji na mazingira kwa shughuli za uchumi ambazo zinafaida kwa watu wachache.

Dkt Mpango amesema kuwa viongozi wa aina hiyo hawafai katika jamii hivyo serikali haiwezi kuwafumbia macho watu kama hao ambao wanaangamiza jamii nyingine kwa makusudi.

Makamu wa Rais amesema kuwa madhara ya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji yamekuwa makubwa na jamii inaathirika kiuchumi,kiafya hata kielimu kwa ajili ya watu wachache wanaoharibu mazingira.

“Sasa hivi viongozi na wananchi wanaoharibu mazingira na vyanzo vya maji watakunywa sumu wenyewe na sio jamii yote hilo swala serikali imelichukulia kwa umuhimu mkubwa”amesema Mpango

Dkt Mpango amesema kuwa jamii,wadau na viongozi wa serikali wanatakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano kuhakikisha wanakomesha swala la uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji ili kuikomboa jamii na madhara ya uharibifu wa mazingira.

Amesema kuwa bonde la Ihefu ni muhimili wa mabwawa ya Mtera,Kidatu na Mwalimu Nyerere hivyo watu wanaohujumu upatikaji wa maji kutoka kwenye hilo bonde hatua kali zitachuliwa.

Dkt Mpango ameitaka mamlaka ya bonde la Rufiji kwenda kubomoa mabwawa yote ambayo yanahifadhi maji kinyume na sheria na kuwataka wampeleke vibali vyote vya matumizi ya maji walivyo vitoa ili aweze kuvipitia na kujua vilitokaje.

Amesema kuwa madhara yamekuwa makubwa sana kwani mwaka 1980 uharibifu ulikuwa asilimia 42,mwaka 2012 uharibifu ulikuwa asilimia 50 na mwaka 2018 uharibifu ulikuwa asilimia 63 hivyo hali inaendelea kuwa mbaya kila kukicha.

Dkt Mpango amesema kuwa suala la familia kumi na mbili kumiliki lanchi atalifanyia kazi haraka sana kwa kufuata taratibu na sheria ili kila moja aweze kupata haki kwa kutumia vyombo husika.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Philip Mpango amemalizia kwa kuitaka wizara kuandaa bajeti kwa ajili ya kuwapa mafunzo waandishi wa habari ili waweze kuandika habari za mazingira vizuri.

Awali mwenyekiti jukwaa la wahariri Tanzania Deodatus Balile alisema kuwa serikali inatakiwa kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale wananchi wanaoharibu kwa makusudi vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla wake.

Balile alisema kuwa zaidi ya hekari laki nne za misitu nchini zimeharibiwa na baadhi ya wananchi kwa ajili ya maslai yao binafsi hivyo ni lazima kuchukua hatua kali bila kumuogopa mtu.

Alisema kuwa wataalam viongozi mbalimbali wanaidanganya serikali juu ya hali halisi ya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji ilivyo hivyo serikali iwatumie waandishi wa habari kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira pamoja na kutoa habari ambazo zitawafichua waharibifu wote wa mazingira.

“Mheshimiwa makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wataalamu wako wanakudanya juu ya hali halisi ya uharibifu wa kimazingira hivyo wanahabari tupo tayari kufanya kazi hiyo bila vocha na kuwafichua waharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira”amesema Balile

Balile amesema kuwa kwenye bonde la Ihefu kunafamilia ya watu kumi na mbili ambao inahusika kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji katika bonde hilo.

Previous Post Next Post