DKT.KISENGE AHIMIZA USHIRIKIANO KUTOKA HUDUMA BORA

 

Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo akitoa taarifa ya kazi zilizofanywa na Taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2022 katika kikao cha wafanyakazi wa JKCI kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akijibu swali katika kikao cha wafanyakazi wa Taasisi hiyo kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete JKCI wakisikiliza kwa umakini uwasilishwaji wa taarifa ya kazi zilizofanywa na Taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2022 katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Picha na JKCI

………………………………..

Na Salome Majaliwa – JKCI

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amehimiza kuimarisha ushirikiano kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo ili waendelee  kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa.  

Dkt. Kisenge alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika katika  ukumbi wa mikutano wa  Taasisi hiyo.

Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kila mfanyakazi anatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kujituma  katika eneo lake la kazi kwa kufanya hivyo wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo wataweza kupata huduma iliyo bora na kwa wakati.

“Licha ya kufanya kazi kwa bidii na weledi tunatakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano kwa maana  wafanyakazi wote tunahitajiana na kutegemeana hivyo basi tuboreshe huduma kwa kutoa huduma bora kwa wateja wetu ili huduma zetu ziendelee kutanuka zaidi na kujulikana mpaka nchi ya nje,” alisema Dkt. Kisenge.

Kuhusiana na kuboresha maslahi ya wafanyakazi  Dkt. Kisenge alisema menejimenti ya Taasisi hiyo imekuwa ikijitahidi kuhakikisha wafanyakazi wanalipwa maslahi yao kwa wakati ili kuwapa motisha ya kufanya kazi zaidi na kuboresha maisha yao.

“Tutaendelea kuboresha hali za wafanyakazi na hapa JKCI kwani kila mfanyakazi ana umuhimu wake kuanzia mfanyakazi wa chini hadi wa juu wote hao malipo yao yatazingatiwa, mimi kama Mkurugenzi Mtendaji naahidi kulifuatilia swala hili kwa umakini wa hali ya juu sana ili kila mfanyakazi alipwe kwa wakati malipo yake na  stahiki,” alisisitiza Dkt. Kisenge.

Akisoma taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2022 Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi Dkt. Delilah Kimambo alisema huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wagonjwa zimekuwa zikiimarika hii ni kutokana na Serikali kununua mashine za  kisasa katika Taasisi hiyo pamoja na wafanyakazi kuwa na ujuzi wa kuweza kuzitumia mashine hizo.

“Wafanyakazi wa JKCI tunapaswa kuwa makini katika kutoa huduma kwa wateja kwa kufanya hivyo wagonjwa wengi watakuja kutibiwa katika Taasisi yetu na hivyo kuweza kutimiza mpango mkakati tuliojiwekea wa kutoa huduma bora za ubingwa bobezi za matibabu ya moyo hapa nchini,”.

“Tutoe huduma nzuri kwa wateja wetu ili waridhirike na huduma tunazozitoa na pia waendelee kuja kutibiwa katika Taasisi yetu kwa kufanya hivi tutakuwa tumewasaidia watanzania pamoja na jirani zetu kutoka nje ya Tanzania wenye matatizo ya moyo kupata huduma za matibabu hapa nchini,”alisema Dkt. Delilah.

Nao wafanyakazi wa Taasisi hiyo waliishukuru menejimenti ya JKCI kwa kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira yanayoridhisha hii ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi, kuboresha maslahi yao  pamoja na kulipia ada za wafanyakazi ambao wanasoma katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi jambo ambalo limewafanya waongeze ujuzi katika taaluma zao.

Previous Post Next Post