Na Mapuli Kitina Misalaba
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amewasihi wazazi, walezi na jamii nzima kuhakikisha wanawalea watoto katika misingi ya utu, upendo na maadili mema, ili vitendo vya ukatili visiendelee kutokea.
Askofu Sangu ametoa wito huo wakati wa mahubiri yake, katika Misa ya kumbukumbu ya watoto Watakatifu wafiadini, ambayo imefanyika kijimbo katika Kanisa kuu la Mama mwenye Huruma Ngokolo mjini Shinyanga, tarehe 28 Desemba 2022, ambapo kupitia maadhimisho hayo, amepata nafasi ya pekee ya kusali, kuzungumza na kula chakula pamoja na watoto kutoka Parokia na Parokia teule zote za jimbo.
Askofu Sangu amewataka Waamini Wakatoliki pamoja na jamii nzima kuungana kwa pamoja kukabiliana na vitendo vyote vya ukatili kwa watoto, kwa kuwa vina madhara makubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho. “Ili Kubomoa misingi ya Ukatili, ni lazima kuwalea watoto katika mazingira ya Utu,Upendo na Maadili Mema”. Askofu Sangu amesisitiza.
Akifafanua zaidi amebainisha kuwa, watoto wanaolelewa katika mazingira ya ukatili huendeleza vitendo hivyo pale wanapokuwa watu wazima, kwa sababu mbegu ya ukatili itakuwa imepandikizwa na kukua ndani mwao tangu utotoni.
Aidha, Askofu Sangu ametumia nafasi hiyo kuwaasa watoto kuwaheshimu wazazi kama njia ya kumtangaza Kristo, ambaye ni upendo, pamoja na kuwapenda na kuwatendea mema watu wengine.
Awali, Askofu Sangu alipokea maandamano ya watoto ambayo yalianzia katika Kanisa la Moyo Safi wa Maria Parokia ya Shinyanga mjini na kuishia katika makazai ya Askofu yaliyopo Kanisa kuu la Ngokolo, ambayo yalikuwa yamebeba ujumbe maalum wa kupinga ukatili kwa watoto.
Akielezea juu ya umuhimu wa maadhimisho hayo, Askofu Sangu amesema kuwa, Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga limeamua kuunganisha maadhimisho hayo ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 28 Desemba, ili kukumbuka watoto waliouawa kikatili na Mfame Herode zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita akiwa na lengo la kumwangamiza mtoto Yesu, hivyo kinyume na Mfalme Herode Kanisa Katoliki Shinyanga limeamua kupaza sauti likiwa na ujumbe maalum wa kupinga ukatili kwa watoto, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono Juhudi za kukabiliana na vitendo hivyo zinazofanywa na Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na wandamizi wake.
Kwa mujibu wa maandiko matakatifu, Mfalme Herode alitoa amri ya kuuawa kwa watoto wote wa kiume wa kuanzia umri wa miaka miwili, kama njia ya kulinda ufalme wake wa Yudea kwa kuamini kuwa, huenda mtoto Yesu aliye tajwa kuwa mfalme na wataalam wa nyota (Mamajusi) kutoka Mashariki angemnyang’anya ufalme wake.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Shinaga ACP Janeth Magomi ambaye alikuwa mgeni maalumu katika maadhimisho hayo, amewakumbusha wazazi, walezi na jamii nzima kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya maovu wanayofanyiwa, pamoja na kuwapa haki sawa bila kuwabagua kwa misingi ya kijinsia.
Maadhimisho hayo ya kumbukumbu ya Watoto watakatifu wafiadini yamewashirikisha watoto zaidi ya 2,000 kutoka Parokia 37 na Parokia teule 3 za jimbo la Shinyanga wakiwemo Mapadre, Watawa na Waamini.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kijimbo inasema kuwa “UKATILI KWA WATOTO SASA MWISHO”