MAAFISA TARAFA WATAKIWA KUTUMIA VIZURI MUDA WA KAZI KUWAHUDUMIA WANANCHI


Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka Maafisa Tarafa 48 waliohudhuria mafunzo ya kujengewa uwezo kiutendaji, kuutumia vizuri muda wa kazi katika kuwahudumia wananchi kama ambavyo Serikali imekusudia.

Bw. Daudi ametoa wito huo kwa Maafisa Tarafa hao jijini Dodoma, wakati akifunga mafunzo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI ili waendane na kasi ya utendaji kazi ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Bw. Daudi amewataka Maafisa Tarafa kutotumia muda wa kazi katika mitandao ya kijamii wakati wana jukumu la msingi la kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi katika maeneo yao ya kazi.

Bw. Daudi ameongeza kuwa, ofisi yake imeshirikiana na TAMISEMI kuandaa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Maafisa Tarafa, kwa kutambua kuwa maafisa hao ni kiungo muhimu kati Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma.

“Ninyi ni kiungo kikubwa cha kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo ukisikia Serikali inalaumiwa kwa kutotoa huduma bora kwa wananchi au kupongezwa kwa kutoa huduma bora ninyi Maafisa Tarafa mnahusika, na ndio maana tumeamua kuwapatia mafunzo ili mkatekeleze majukumu yenu kikamilifu,” Bw. Daudi amefafanua.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI amewataka Maafisa Tarafa kusimamia nidhamu katika Utumishi wa Umma kwa ngazi ya tarafa kwani Sheria inamtambua Afisa Tarafa kuwa ni mwakilishi wa Afisa Tawala wa Wilaya kwenye ngazi ya tarafa ambapo moja ya jukumu la Afisa Tawala Wilaya ni kuhakikisha mamlaka zote za Serikali kwenye ngazi ya wilaya zinatimiza majukumu ya kiutumishi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya utumishi wa umma iliyopo.

Naye, Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Edith Rwiza amesema, mafunzo kwa Maafisa Tarafa hao yametolewa kwa siku mbili yakilenga kuwajengea uwezo Maafisa Tarafa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora na endelevu kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Tarafa waliopatiwa mafunzo, Bw. Titho Cholobi ambaye ni Afisa Tarafa wa Elerai Wilaya ya Arusha amesema kuwa mafunzo waliyopatiwa yamewawezesha kuzaliwa upya kiutendaji na kuongeza kuwa, yeye binafsi mafunzo hayo yamemuwezesha kubaini mapungufu aliyokuwa nayo katika utendaji kazi wake.

Previous Post Next Post