MANJERENGA AWATAKA WAFUGAJI WA MIFUGO MANISPAA YA SHINYANGA KUFUATA MAELEKEZO YA SERIKALI

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Afisa Maliasili anayesimamia uhifadhi rasilimali mazingira katika Manispaa ya Shinyanga Ezra Manjerenga amewataka wafugaji wa mifugo kufanyia ufugaji kwenye maeneo yao ili kuepuka uhalibifu wa Mazingira hasa miti iliyopandwa kwa manufaa ya mji wa Shinyanga.

Ametoa rai hiyo leo wakati akitoa elimu na ukaguzi kwa wafugaji wa Mifugo aina ya Ng’ombe na Mbuzi mtaa wa Magadula kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga.

Mhifadhi Mazingira Manjerenga amewasisitiza wafugaji wa mifugo kuzingatia sheria na taratibu zilizopo ambapo amesema Halmashauri hiyo itaenedelea kuchukua hatua mbalimbali kwa wafugaji wanaoonekana mifugo wao kuzurura katika maeneo yaw engine.

“Hakikisha kwamba eneo ulilopangiwa la makazi iwe ni 30 kwa 40 au 20 kwa 10 hilo ndiyo eneo lako ambalo unatakiwa wewe kulitumia katika mambo yako yote ya kifamilia ikiwemo ufugaji”.

“Ufugaji unaoruhusiwe ni ufugaji wa ndani kwahiyo mfugo unaotoka nje ya eneo ambalo wewe umepangiwa huo siyo mfugo ambao tutauvumilia kwa sababu unakotoka unaenda kuharibu maeneo ya watu wengine kwahiyo niendelee kuwasisitiza sana wafugaji wa Manispaa ya Shinyanga wafuge wakiangalia mifugo yao hasa mifugo inayoachiwa hovyo na kuzurura na sisi  Halmashauri baada ya kutoa elimu hii mifugo wote ambao wataonekana kuzurura tutawakamata, kwa miti ambayo imeliwa na mbuzi mara  nyingi ukuwaji wake niwa kudumaa na mingi inakufa”.amesema Manjerenga

Baadhi ya wananchi wafugaji katika mtaa huo wa Magadula wameahidi kutekeleza maelekezo ya serikali huku wakiomba kutengewa maeneo yao rasmi kwa ajili ya kuendeleza ufugaji wao.

Aidha afisa Maliasili na Mazingira Manispaa ya Shinyanga Ezra Manjerenga wakati akizungumzia suala hilo ameshauri kutengeneza vikundi maalum vya wafugaji na kuonana na viongozi husika wa Halmashauri ili kupata eneo la kufugia.

Manjerenga pia amewakumbusha wakazi wa Manispaa ya Shinyanga kuendelea kupanda miti hasa kwenye nyakati hizi za msimu wa mvua ili kuandaa mazingira katika hali nzuri ya kupendezesha mji ambapo amesema miti inatolewa bure kwa yoyote atakae hitaji.

 

Naye Mwenyekiti wa wenyeviti Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni mwenyekiti wa mtaa wa Mjini Nassor Mkh Worioba akiwa ameambatana katika zoezi hilo amepokea ombi la wafungaji na kuahidi kwenda kulifanyia kazi baada ya kuomba mkutano wa wafugaji na viongozi wa serikali.

“Mimi kama Mwenyekiti wa wenyeviti Manispaa ya Shinyanga jambo la kufanya mkutano naondoka nalo nitawaagiza wenyeviti wangu wa kata ya Ngokolo kuitisha kikao cha wafugaji wote wa kata hii ili tukutane wapokee yetu na sisi tupokee yao ili kufika sehemu nzuri tunapohitaji lakini pia tutashirikiana na maafisa mifugo ambao watakuja pia kutoa elimu”

“Lakini  na mimi niwashauri  wafugaji wote wa Manispaa ya Shinyanga tujitahidi kufuga mifugo yetu ndani tusiwafungulie na kuzagaa hovyo na kula miti yetu nashauri sana tufugie ndani na chakula tuwapelekee humo ili kuepukana na madhara”.amesema Mwenyekiti Worioba

Afisa Maliasili anayesimamia uhifadhi rasilimali mazingira katika Manispaa ya Shinyanga Ezra Manjerenga akizungumza na mama mfugaji wa Mbuzi wa mtaa wa Magadula kata ya Ngokolo.

Mwenyekiti wa wenyeviti Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni mwenyekiti wa mtaa wa Mjini Nassor Mkh Worioba akizungumza wakati wa zoezi la ukaguzi likiendelea.

Mti ulioliwa na mifugo katika mtaa wa Magadula kata ta Ngokolo.



Previous Post Next Post