RAIS DKT. SAMIA ATOA ZAWADI YA XMASS KWA WATOTO YATIMA

 


Baadhi ya watoto yatima katika kituo cha Chipole wakipokea zawadi na mbuzi wanne waliotolewa na Rais Dkt.Samia kwa ajili ya sikuu za mwisho wa mwaka 2022 

Miongoni mwa watoto yatima wa kituo cha Chipole wilayani Songea ,kituo hicho kinalea  watoto yatima 72.

***************

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi ya Sikukuu za mwisho wa mwaka kwa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Chipole wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Akikabidhi zawadi hizo Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Mheshimiwa Pololet Mgema amesema Mheshimiwa Rais ametoa zawadi kwa kituo hicho kwa niaba ya vituo tisa vilivyosajiriwa  vya Watoto wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Ruvuma.

“Mheshimiwa Rais anaungana na Watoto wa kituo cha Chipole kwa kuwatakia kheri ya sikukuu kwa kutoa mchele kilo 100,mbuzi wanne,maharage kilo 40,mafuta ndoo moja na viungo ambavyo vyote vimegharimu shilingi 1,150,000’’,alisema RC Thomas.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa zawadi aliyoitoa kwa Watoto yatima Chipole ambapo amesema huo ni upendo wa hali ya juu wa kuwakumbuka wenye mahitaji ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi .

Akitoa taarifa ya kituo hicho kwa niaba ya Watoto wenzake mtoto Maria Mkange amesema kituo hicho kilianzishwa mwaka 1963 kikiwa na lengo la kuwasaidia Watoto wachanga ambao wamefikiwa na wazazi wao.

Hata hivyo amesema hadi sasa kituo hicho kina Watoto yatima 72  kati yao wavulana 41 na wasichana 31.Amesema wanamshukuru Rais kwa upendo wake kwao hasa wa kuwapatia zawadi katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Bakari Mketo amewapongeza watawa wa Shirika la Mtakatifu Agnes Chipole ambao ndiyo wamiliki wa kituo hicho kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulea Watoto yatima.

Amesema kazi inayofanywa na watawa hao ni ya kutukuka na malipo ambayo  watayapata mbele ya mwenyezi Mungu ni makubwa, amewatia moyo  kuendelea na kazi hiyo ngumu ya kulea Watoto yatima.

Previous Post Next Post