Pamoja na mjadala huo, miradi hiyo inayotarajiwa kukuza uchumi wa Taifa, ipo katika hatua nzuri na leo Bwawa la Julius Nyerere likianza kujazwa maji kwa ajili ya usalishaji umeme, huku Serikali ikifafanua kuwa kauli zote mbili ni sahihi.
Wakati miradi hiyo inaanza kutekelezwa, Dk John Magufuli aliyekuwa Rais wa awamu ya tano alikuwa anasema kila kitu kinafanywa kwa fedha za ndani akisisitiza Tanzania ni tajiri na inaweza kujisimamia.
Lakini mrithi wake, Rais Samia Suluhu Hassan anasema Serikali inakopa ili kujenga miradi hiyo, kwa kuwa isingeweza kufanya hivyo kwa kutumia fedha za ndani.
Uwazi wa Rais Samia, aliyekuwa makamu wa Rais enzi za hayati Magufuli unazua mjadala katika mitandao ya kijamii kutokana na kurekebisha baadhi ya kauli za mtangulizi wake kuhusu miradi ya kitaifa inayotekelezwa katika maeneo tofauti.
Katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kwa mfano, Rais Magufuli alikuwa anasema gharama zake zinalipwa kwa mapato ya ndani kwa asilimia 100.
Aprili 12, 2017 wakati anazindua awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, hayati Magufuli alisema ilikuwa ni mara ya kwanza kwa nchi kugharamia ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa kwa fedha za ndani.
“Kutumia fedha za walipa kodi ni hatua inayoakisi uwezo wa baadhi ya nchi za Afrika kugharimia miradi mikubwa ya maendeleo bila kutegemea wahisani,” alisema.
Hata Novemba 29, 2015 alipofuta sherehe za uhuru kama njia ya kubana matumizi, alielekeza Sh4 bilioni za maadhimisho hayo zitumike kuitanua barabara kutoka Morocco mpaka Mwenge, jijini Dar es Salaam.
Lakini Desemba 5, 2021 Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema barabara hiyo ilijengwa kwa Sh71.8 bilioni zilizotolewa msaada na Japan.
Julai 2019 alipoweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme nao, Dk Magufuli alisema ujenzi huo ungegharimu Sh6.5 trilioni kutoka katika mapato ya ndani.
Hata hivyo, imekuja kufahamika kuwa ukopaji huo kwa ajili ya miradi mbalimbali umesababisha deni la Taifa lipande na kufika zaidi ya Sh91.7 trilioni, jambo ambalo Rais Samia anaweka bayana kuwa Serikali imekopa ili kutekeleza miradi ya maendeleo kwan kuwa isingewezekana kufanya hivyo kwa kutegemea mapato ya ndani.
Akizungumza juzi wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi wa SGR kipande cha kutoka Tabora hadi Kigoma, Rais Samia alisema uwekezaji wa Sh23.3 trilioni kwenye reli hiyo ni mkopo, kwani bila hivyo isingejengwa.
“Hizi Sh23.3 trilioni au dola 10.04 bilioni zote ni mkopo. Wale wanaosema awamu hii imekopa sana wajue kuwa ndiyo awamu ambayo imejenga reli na tusingeweza kujenga kwa fedha za ndani. Ilibidi tukope,” alisema.
Tutuba mkuu afafanua
Ili kupata ufafanuzi wa kauli hizo za marais wawili kuhusu jambo hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema ni kweli fedha zinazotumika ni za Watanzania.
“Kwenye kila bajeti ya Serikali huwa kunakuwa na upungufu ambao tunaujaza ama kwa kukopa au kutumia fedha za wafadhali. Bila kujali zitatoka wapi, zikiingia huwa zinakuwa za Watanzania, ndipo zinatumika. Ni sahihi kusema miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa fedha za Watanzania, kwani hata wewe ukikopa ukajenga nyumba utasema umejenga kwa fedha zako, si ndiyo?” alisema Tutuba.
Alipoulizwa kuhusu barabara ya kutoka Morocco mpaka Mwenge, Tutuba alisema ujenzi wake ulifanywa kwa awamu mbili tofauti, kwanza kwa fedha za Serikali halafu kwa ufadhili wa Japan (Jica).
“Jica walifanya upembuzi yakinifu ila wakachelewa kutupatia fedha kwa miaka kama saba hivi, ndiyo maana Rais (Magufuli) akaona tuanze kwa fedha zetu ili wakileta wakute tumeshaanza,” alisema.
Fedha za Serikali, alisema ziliongeza njia moja kila upande na za Jica zilipokuja zikaitanua zaidi barabara hiyo.
“Ulikuwa ni uamuzi sahihi wakati ule kwa sababu kipande cha kutoka Morocco mpaka Mwenge kilikuwa na njia moja kila upande wakati ile inayotoka Tegeta mpaka Mwenge inazo mbili (kila upande) na kuanzia Morocco kuja mjini zipo mbili pia.
“Hicho kipande kilikuwa na foleni kubwa sana,” alisema Tutuba, akifafanua kuwa fedha za ndani ziliongeza njia moja kila upande na za Jica zikaitanua zaidi.
Fedha za ndani hazitoshelezi
Akizungumzia uamuzi wa Serikali kukopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Lawi Yohana alisema ni sawa iwapo fedha za ndani hazitoshelezi.
“Serikali huwa na mipango mingi, sasa inapotokea fedha za ndani ni haba hulazimika kukopa. Kwa makadirio, TRA inakusanya wastani wa Sh2 trilioni kila mwezi, kati ya hizo Sh800 bilioni zinalipa mishahara, Sh900 bilioni zinalipa madeni. Hapo tunabakiwa na Sh300 bilioni ambazo haziwezi kutekeleza miradi mikubwa, hivyo lazima ukope,” alisema.
Dk Lawi alisema mkanganyiko ni vile Serikali ilisema inatumia fedha za ndani lakini kiuhalisia haina mapato makubwa ya kufanya miradi mikubwa kwa fedha zake.
“Ilikuwa lugha ambayo haikuwa na ufafanuzi mzuri, awamu ya tano ilikuwa inamaanisha fedha zile zitalipwa. Kimsingi ile pia ilikuwa ni mikopo,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Aurelia Kamuzora, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, alisema nchi kama Tanzania kutumia fedha za ndani pekee kunaweza kusababisha kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi kwa kuwa inao mtaji mdogo.
“Kama fedha zipo kweli na ukizitumia kwenye miradi ya maendeleo, nchi itanufaika zaidi kwa sababu haitatakiwa kulipa riba inayokuwapo kwenye kila mkopo. Kukopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kuna faida kubwa, hasa kuchochea kasi ya ukuaji uchumi kwenye jamii,” alisema.
“Wachumi tulijua miradi hii inatekelezwa kwa mikopo. Awamu ya tano ilitumia mikopo ya ndani kwa kuuza dhamana (bonds) za Serikali, hapa ilikuwa inakopa kutoka kwa wananchi wake,” alisema Kamuzora.
Hata hivyo, Dk Richard Mbunda, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema taswira za kutekeleza miradi ya maendeleo zimekuwa tofauti kati ya awamu ya tano na ya sita kwa sababu viongozi wametofautiana falsafa.
“Falsafa za utawala wa awamu ya tano ilijipambanua kuwa inaweza kufanya mambo yenyewe na kuuchukia ubeberu, lakini awamu ya sita inaamini ili uweze kuendelea lazima ushirikiane na wadau wa maendeleo,” alisema mhadhiri huyo.
Dk Mbunda alisema katika awamu iliyopita, mikopo ilichukuliwa lakini kutokana na falsafa za Rais aliyekuwepo taarifa hazikutolewa, tofauti na hali iliyopo sasa.
Chanzo - Mwananchi