Ticker

6/recent/ticker-posts

TAKWIMU ZAONYESHA ONGEZEKO LA UVIKO-19

 Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya zimeonyesha ongezeko la wagonjwa wa Uviko-19 nchini kutoka asilimia 4.1 hadi asilimia 5.5.

Takwimu za wiki ya kwanza ya Novemba 2022 zinaonyesha watu 1,154 waliopima Uviko-19, waliokuwa wanaugua ni 47, huku takwimu za wiki ya pili zinaonyesha kati ya watu 1,294 waliopima Uviko-19, watu 71 wanaugua ugonjwa huo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema hayo , wakati akitoa tamko lake la salamu za sikukuu ya Krismasi huku akiwataka watumiaji wa vyombo vya moto kuwa makini barabarani.


“Kwa mujibu wa taarifa zetu, katika kipindi cha kati ya wiki ya kwanza ya Novemba na wiki ya pili ya Desemba 2022 kumekuwa na ongezeko la magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa.

“Ufuatiliaji wa Wizara umeonyesha kuwa visababishi vikuu vya magonjwa haya ni virusi vya Uviko-19 pamoja na virusi wengine wenye kusababisha mafua na kikohozi, mfano virusi vya Influenza (Influenza viruses),” alisema.

Waziri Ummy alisema wagonjwa wa Uviko-19 wameongezeka kutoka asilimia 4.1 hadi asilimia 5.5.

Pia, alisema wagonjwa wa Influenza wameongezeka kutoka asilimia 4.8 hadi asilimia 6.5, huku watu 277 waliopima Influenza katika wiki ya kwanza ya Novemba 2022, waliokuwa wanaugua ni 11.

Takwimu hizo hizo pia katika wiki ya pili ya Desemba zinaonyesha kuwa kati ya watu 155 waliopima, 10 walikuwa wanaugua Influenza.

“Kutokana na hali hii, Wizara inaendelea kuwakumbusha wananchi kuchukua hatua ili kujikinga na magonjwa haya, ikiwamo kupata dozi kamili ya chanjo ya Uviko-19 kwa ambao hawajachanja, kuvaa barakoa pindi mtu anapokuwa na dalili za mafua au kikohozi na awapo kwenye mikusanyiko.

“Kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuzingatia kanuni za afya na usafi binafsi, ikiwamo kujikinga kwa kitambaa au kiwiko cha mkono wakati wa kupiga chafya au kukohoa,” alisema Waziri Ummy.


Wakati huohuo, Serikali imewataka watumiaji wa barabara kuchukua tahadhari katika msimu huu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya ili kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo, ulemavu wa kudumu na kuipa Serikali mzigo mkubwa wa kuhudumia wahanga.

Imebainisha kuwa asilimia 60 ya wagonjwa hao hawana bima ya afya na hushindwa kulipia huduma waliyopata, hivyo Serikali hubeba mzigo huo wa matibabu ambao ni mkubwa kutokana na gharama za vifaa tiba.

“Tuchukue tahadhari ili kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo au ulemavu wa kudumu na kuipa Serikali mzigo mkubwa wa kuhudumia waathirika. Takwimu za Taasisi ya Mifupa za kipindi cha Julai hadi Septemba 2022 zinaonyesha kuwa wagonjwa wa ajali walikuwa 2,410 na kati yao asilimia 70 walikuwa ni wagonjwa kutokana na ajali za barabarani,” alisema Waziri Ummy.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan juzi wakati akitoa salamu zake za sikukuu kwa Watanzania kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii za Twitter na Instagram aliandika; “Panapo majaliwa, siku chache zijazo tutasherehekea sikukuu za Krismasi (leo) na Mwaka Mpya. Nawatakia nyote kheri katika sherehe hizi ili ziwe za furaha na zisizo na misiba inayoweza kuepukika. Nawasihi wasafiri na madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuchukua tahadhari.”



Chanzo - Mwananchi

Post a Comment

0 Comments