VIELELEZO NA VITU IKIWEMO BUNDUKI, PIKIPIKI, VYUMA VYA TANESCO NA DAWA ZA KULEVYA VYAKAMATWA SHINYANGA KAMANDA MAGOMI TUMEJIPANGA MSIMU WA SIKUKUU

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kukamata vielelezo  na vitu mbalimbali ikiwemo Bunduki, Dawa za kulevya pamoja na Pokipiki za wizi na zilizokuwa zikitumika kufanyia uhalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema hatua hiyo inafuatia baada ya kufanya msako na opereshen mbalimbali katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzi Novemba 22,2022 hadi Desemba 12,2022.

ACP Magomi amesema jeshi hili limefanikiwa kukamata vielelezo mbalimbali ikiwemo vifaa vya tiba mbalimbali ambavyo ni mali ya serikali, simu, pangi, Computer pamoja na vyuma vya ujenzi wa minara ya tanesco.

“Tumefanikiwa kukamata vitu na vielelezo mbalimbali kama ifuatavyo vifaa tiba mbalimbali ambavyo ni mali ya serikali, Bunduki moja, ya kiraia aina ya Gobore, Simu janja, 14, Simu ndogo tatu, Pikipiki kumi za wizi au zilizokuwa zikitumika kutendea uhalifu, Dawa za kulevya aina ya Heroine kete kumi, Bangi kete 71, Pombe haramu ya gongo lita 20, Tv Nne, na Mitungi ya gesi miwili”.amesema ACP Magomi

“Vitu vingine ni vyuma vya ujenzi wa minara ya TANESCO, Speaker mbili, Vitenge doti Nne, Computer tatu, Subwoofer Nne, Monitor moja, Gogoro moja, Panga moja, Shoka moja na makabati mawili ya kuhifadhia Chips”

“Tuliokota Pikipiki Nane na Baskeli 11 ambazo katika mazingira tofauti zilisahauliwa na wamiliki wake maeneo mbalimbali au kutupwa kutokana na sababu tofauti kama vile ulevi na mambo mengine kama hayo”..amesema Kamanda Magomi

Kamanda magomi ameeleza kuwa katika kipindi hicho kesi mbalimbali zimefanikiwa ambapo watuhumiwa 31 wa makosa mbalimbali wanashikiliwa na wengine wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ikiwemo mauaji, wizi pamoja na ubakaji.

“Jumla ya kesi 31 tulizipeleka Mahakamani, kesi za mauaji tatu, kesi za kubaka 8, kulawiti 3, ukatili dhidi ya mototo kesi mbili, kujeruhi kesi 2, kuvunja Nyumba usiku na kuiba kesi 1, kupatikana na Bangi kesi 3, wizi wa motto kesi 1, kupatikana na Pombe ya Moshi kesi mbili, kupatikana na Mirungi kesi moja, kumtorosha mototo kesi kesi moja, kumpa mimba Mwanafunzi kesi moja, wizi kesi moja pamoja na wizi wa kuaminiwa kesi moja ambazo zote zilipatiwa hukumu”.amesema Kamanda Magomi

Aidha kamanda Magomi amewataka wakazi wa   Mkoa wa Shinyanga kufuata sheria za Nchi wakati wote na kutojihusisha na vitendo vya kihalifu hususani katika kipindi hiki cha sikukuu za Kristmass na Mwaka mpya kwani jeshi hili limejipanga na wahalifu.

“Nawaasa wananchi, madereva na bodaboda kufuata sheria za Nchi wakati wote na kutojihusisha na vitendo vya kihalifu kwa namna yoyote hususani kipindi hiki cha sikukuu za Kristmass na Mwaka mpya kwani jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga tumejipanga kikamilifu katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu na wahalifu”.

“Tunawaomba wananchi kufika katika kituo kikubwa cha Polisi Shinyanga mjini kwa ajili ya kuzitambua mali zao kuanzia 22.12.2022 hadi 30.13.2022”.amesema ACP Magomi

Aidha kamanda Magomi amesema  upande wa usalama barabarani katika kipindi cha mwezi mmoja hakukuwa na tukio lolote kubwa la barabarani ambapo ameeleza kuwa yalifanyika makosa madogomadogo ya Magari 2796 na makosa ya Pikipiki 937 ambayo yote yalichukuwa hatua za kisheria kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali ikiwemo Mahakama, LATRA, TRA, TONROADS, BIMA, FIRE na Manispaa.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi wakati akisoma taarifa ya mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi hicho.

Pikipiki zilizokamatwa za wizi au zilizokuwa zikitumika kutendea uhalifu.


Previous Post Next Post