WAANDISHI MANYARA WAIPONGEZA SERIKALI KUFANYIA MAREKEBISHO SHERIA KANDAMIZI

 

Mmwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Manyara, (MPC) Zacharia Mtigandi akizungumza kuhusu serikali kukubali kuzifanyia marekebisho sheria na kanuni inazokwaza waandishi wa habari katika kazi zao.
…………………………….
Na Mwandishi wetu, Babati
MWENYEKITI wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Manyara, (MPC) Zacharia Mtigandi ameipongeza Serikali kwa kukubali kuzifanyia marekebisho sheria na kanuni kandamizi zinazozuia vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uhuru.
Mtigandi amesema katika kongamano la habari lililofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliahidi sheria hizo kuanza kufanyiwa maboresho katika kikao kijacho cha Bunge mwaka ujao 2023.
Amesema hatua ya Waziri Nape kuutangazia umma kuwa marekebisho ya kuboresha taaluma ya habari yameshafanyiwa kazi na yatafikishwa Bungeni Januari 2023 ni jambo la kupongezwa.
Amesema wanaipongeza Serikali kwa hatua hiyo kwani wameyasikiliza maoni ya wadau wa habari mahali penye mapungufu na kuyafanyia kazi hivyo ni hatua kubwa.
“Tunaipongeza Serikali kwa hatua hiyo kwani imeonyesha ni sikivu kwa kutekeleza maoni hayo ambayo kwa namna moja au nyingine itaongeza chachu kwa waandishi wa habari,”  amesema Mtigandi.
Amesema inapozungumzwa Serikali sikivu ni kama hivyo yaani unasikiliza maoni ya wadau na kuyafanyia kazi na wanaipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua hiyo.
Mmoja kati ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara, Joseph Lyimo ameeleza kuwa anaishukuru Serikali kwa namna ilivyochukuwa hatua kwenye suala hilo.
Lyimo amesema yapo masuala mengi katika sheria hizo ikiwemo Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 yanahitaji maboresho.
“Marekebisho ya sheria na kanuni hizo ambayo sehemu yake yanatarajiwa kuwasilishwa katika kikao kijacho cha Bunge ni ya msingi ambayo yanapaswa kutizamwa kwa jicho la tatu,” amesema Lyimo.
Amesema baadhi ya vifungi vinavyolalamikiwa kwenye Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 pamoja na mambo mengine, inaruhusu Serikali kufungia magazeti.
Sheria hiyo pia inaweka sharti kwa gazeti kuwa na leseni ambayo inapaswa ihuishwe kila mwaka.
Amesema kingine kinacholalamikiwa ni Kanuni za Mawasiliano na Kielektroniki na Posta, Maudhui ya Mtandaoni za 2020 ambazo pamoja na kuipa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kufungia redio, runinga na vyombo vya habari vya mtandaoni kwa kukiuka vitu kama vile “maadili ya taifa” pia zinaweka sharti kwa vyombo vya mtandaoni kuwa na leseni inayohuishwa kila mwaka ambayo gharama yake imekuwa ikilalamikiwa na wadau.
Amesema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupokea malalamiko ya wadau kuhusu sheria hizo na kuagiza zianze kufanyiwa marekebisho ili kuweka mazingira bora kwa wanahabari kufanya kazi zao.
Previous Post Next Post