ASKOFU SANGU AWASHUKURU WAZAZI NA WALEZI SHINYANGA
Misalaba0
Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amewashukuru wazazi na walezi ambao wamekubali watoto wao wayatolee maisha yao kwa ajili ya kumtumikia Mungu na Kanisa, kupitia shirika jipya la kijimbo la Mtakatifu Bikra Maria Mama mwenye Huruma.
Askofu Sangu ametoa shukrani hizo katika Misa ya kufunga nadhiri za kwanza za kitawa kwa Wanovisi sita na kurudia nadhiri kwa Masister wawili wa Shirika hilo la Jimbo la Shinyanga, iliyofanyika Januari 1, 2023, katika Kanisa kuu la Mama mwenye Huruma Ngokolo mjini Shinyanga.
Amesema hayo yamewezekana kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na wazazi pamoja na walezi ya kuwalea katika misingi ya imani, uadilifu na maadili mema, hatua ambayo imewasaidia watawa hao wapya kutambua karama na wito wao wa kumtumikia Mwenyezi Mungu.
Amewataka wazazi na walezi kuendelea kupalilia misingi ya miito, ili Kanisa la Mungu liweze kuendelea kupitia miito na karama mbalimbali pamoja na kutambua kuwa, maisha ya hapa duniani ni ya kupita, bali maisha ya mbinguni ni ya milele, hivyo yanapaswa kupaliliwa.
Askofu Sangu amewapongeza watawa waliofunga nadhiri zao za kwanza pamoja na wale waliorudia nadhiri na kubainisha kuwa, wamefikia hatua hiyo huku wakiwa wamepitia changamoto mbalimbali ambazo waliweza kuzivumilia na kushinda.
Amewataka Watawa hao kuishi maisha ya sala na ibada, huku wakitambua kuwa, maisha ya kitawa hapa duniani yanatoa sura ya maisha ya mbinguni ambako hawaoi wala kuolewa.