ASKOFU SANGU AWATAKA WAAMINI WAPYA KUYASHIKA MAFUNDISHO YA IMANI, PAROKIA YA LUBAGA- SHINYANGA
Misalaba0
Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amewapongeza Waamini wa Parokia ya Lubaga kwa moyo wao wa majitoleo, hatua ambayo imewezesha wanunue eneo lenye ukubwa wa Hekari 4 kwa ajili ya ujenzi wa Kigango cha Bushushu.
Akizungumza baada ya kufanya ziara ya kichungaji ya siku moja katika Parokia hiyo, amesema kupitia moyo wa majitoleo ambao wanaufanya Waamini wa Parorokia hiyo ya Lubaga, wanapata baraka nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kujiwekea hazina mbinguni, baada ya maisha yao ya hapa duniani.
Amewasihi kuendelea kusali ili Mungu awawezeshe kuliendeleza eneo hilo, ambapo pamoja na kujenga Kanisa, pia waweze kujenga nyumba ya Watawa pamoja na huduma nyingine za kijamii, ikiwemo shule ya awali.
Askofu Sangu amebainisha kuwa, eneo hilo lina mchango mkubwa katika kusogeza huduma za kiroho kwa watu, na anatamani kuona siku moja Bushushu inakuwa Parokia mpya.
Aidha, Askofu Sangu amempongea Diwani wa Kata ya Lubaga Bw. REUBEN DOTTO, kutokana na juhudi alizozifanya katika kufanikisha kupatikana kwa eneo hilo, na amemtunuku hati maalum ya kutambua mchango wake kwa kanisa.
Wakati huohuo, amewataka Waamini wapya aliowapa Sakramenti ya Kipaimara kuyashika mafundisho yote ya imani waliyopewa, pamoja na kuishi kwa wema, upendo, amani na maadili mema.
Akiwa Katika Parokia hiyo ya Lubaga kwa ziara ya siku moja, ambayo imefanyika Jumapili tarehe 07.01.2023, Askofu Sangu ameweka jiwe la msingi na kubariki katika eneo ambako kutajengwa Kigango cha Bushushu, kuwaimarisha Wakristo wapya 103, kubariki ndoa 39 zilizodumu kwa miaka mitano na kuendelea pamoja na kupokea michango ya kulitegemeza Jimbo iliyochangwa na Waamini wa Parokia hiyo.