Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, leo Jumapili tarehe 08.01.2023, atafanya ziara ya kichungaji katika Parokia ya Lubaga mjini Shinyanga, ambapo pamoja na mambo mengine, atawaimarisha Wakristo wapya wapatao 103.
Kwa mujibu wa Paroko wa Parokia ya Lubaga Padre James Misana, Askofu Sangu atapokelewa majira ya 2:00 asubuhi katika eneo la Bushushu, ambako ataweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Kigango cha Bushuhu, pamoja na kubariki eneo hilo.
Baada ya kurudi makao makuu ya Parokia ya Lubaga katika Kanisa la Mtakatifu Yohane Paul wa Pili , Askofu Sangu ataongoza Misa ya Kipaimara ambayo itakwenda pamoja na kubariki ndoa ambazo zimedumu kuanzia miaka mitano na kuendelea, na atapokea michango ya kulitegemeza jimbo ambayo imechangwa na Waamini wa Parokia hiyo.