Baada ya kupuliza kipyenga kuwaruhusu wanachama na makada wake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi katika chaguzi zijazo kuanza kutia nia, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza uamuzi wa kuanza maandamano ya amani na mikutano ya hadhara kuanzia Januari 5, mwaka huu.
Tangazo la kuruhusu wenye nia ya kugombea kuanza kutia nia na la maandamano na mikutano ya hadhara limetolewa kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika inayoendelea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mnyika yuko kwenye ziara ya Kanda ya Ziwa tangu Desemba 27 mwaka jana na inatarajiwa kukamilika Januari 9, mwaka huu na atatembelea Mwanza, Geita, Shinyanga na Kagera.
Akizungumza na viongozi na makada wa Chadema kutoka Wilaya za Ilemela na Nyamagana Desemba 29, mwaka jana, Mnyika alisema kutia nia mapema kutatoa fursa kwa chama kupima uwezo wa wagombea wake kabla ya kuingia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwakani na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Alitaja miongoni mwa vipimo vitakavyotumika kutambua uimara na uwezo wa wagombea ni jinsi wanavyoshiriki na utimamu wao katika kujenga chama kwa kuingiza wanachama wapya.
Alisema madai ya Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi ni mambo ya msingi na kiini cha ushindi katika chaguzi zijazo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na mbunge wa zamani wa Tarime vijijini, John Heche aliyeahidi kuongoza mikakati ya kurejesha viti vya ubunge katika majimbo ya Ilemela, Ukerewe, Tarime Mjini na Vijijini, Bunda, Serengeti na Nyamagana yaliyokuwa yakiongozwa na Chadema kabla ya kunyakuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Maandalizi ya maandamano
Katika mkutano uliofanyika juzi mjini Kahama, Chadema walitangaza mkakati wa kuanza kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia Januari 5, mwaka huu bila kujali iwapo mchakato wa mwafaka kati yake na CCM utakamilika au la.
Tangazo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Gimbu Masaba, akiungwa mkono na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Pambalu wakisisitiza kuwa ni haki ya kikatiba na kisheria kwa vyama vyote kufanya shughuli halali za kisiasa, ikiwemo mikutano ya hadhara na maandamano ya amani.
“Muda ukifika, vijana na wana Chadema wote tujitokeze kushiriki shughuli halali za chama kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi, wale wenye hofu na woga wasikae mbele yetu, watatuchelewesha, watupishe sisi wenye uthubutu katika jambo la haki tusonge mbele,” alisema Pambalu
Wadau wengine wa siasa
Akizungumzia mikutano ya hadhara na maandamano ya amani ya kisiasa iliyozuiwa tangu mwaka 2016, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza ahadi yake ya kufanya mageuzi ya kisiasa kumaliza mdororo wa usatawi wa demokrasia uliodumu kwa miaka saba sasa kutokana na zuio la mikutano ya hadhara.
“Tumekuwa na miaka saba ya kiza kinene kisiasa baada ya mikutano na shughuli halali za kisiasa kuzuiwa, Rais Samia ameonyesha njia kwa kutoa ahadi ya kuondoa mdororo wa ustawi wa demokrasia, ni vema sasa itolewe ratiba ya utekelezaji wa ahadi yake,” alisema Shaibu.
Alitaja mambo manne yanayohitaji ratiba ya utekelezaji kuwa ni mageuzi ya kisiasa, Tume Huru ya Uchaguzi, mchakato wa Katiba mpya, mageuzi, muundo na utendaji wa Jeshi la Polisi, hasa katika masuala ya haki jinai na demokrasia.
Katibu Mkuu wa chama cha ADA-TADEA, John Shibuda alisema anaamini shughuli na mikutano ya kisiasa itaanza muda si mrefu kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM ameonyesha nia njema ya kujenga na kuimarisha demokrasia kwa kuunda kamati kukusanya maoni na kufanya mazungumza na vyama vya siasa kutafuta mwafaka kwenye matatizo.
“Bila CCM imara na madhubuti hakuna demokrasia. Rais Samia kupitia nafasi yake ya uenyekiti wa CCM ameanza kujenga mfumo wa kuwa na CCM imara isiyotegemezi kwa vyombo vya dola kama ilivyo enzi za Tanu wakati wa kudai na kupigania uhuru,” alisema Shibuda, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la vyama vya siasa nchini.
Heche alia bomoabomoa
Mbunge wa zamani wa Tarime vijijini, John Heche amemwomba Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko, kuingilia kati bomoabomoa ya nyumba za wakazi wa kijiji cha Komarera Wilaya ya Tarime mkoani Mara, kupisha shughuli za uchimbaji madini za mgodi wa Barrick North Mara.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, Heche ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema bomoabomoa hiyo siyo tu imekumba hadi baadhi ya nyumba zenye zuio la Mahakama, bali pia inahusisha nyumba za watu ambao ama hawajalipwa fidia au fidia yao ni ndogo kulinganisha na thamani ya mali zao.
“Hivi tunavyozungumza wapo wanawake, watoto na wazee wanalala nje kwa kukosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa chini ya ulinzi wa vyombo vya dola; namsihi Waziri wa Madini, ndugu yangu Dotto Biteko aingilie kati suala hili, maana linaelekea kuushinda uongozi wa Serikali Wilaya ya Tarime na Mkoa wa Mara,” alisema Heche.
Akizungumzia ombi hilo, Dk Biteko alisema suala hilo tayari linafanyiwa kazi kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mujibu wa sheria na kuwasihi wananchi wenye malalamiko kutumia njia sahihi kuyawasilisha katika mamlaka husika kwa utatuzi.
“Suala la fidia Nyamongo liko chini Wizara ya Ardhi na tayari mchakato unaendelea, ikiwemo tathmini ya mali na malipo kwa wahusika kwa mujibu wa sheria. Kama kutakuwa na hitaji la wizara nyingine kusaidia Serikali itafanya hivyo kwa ajili ya kutoa haki kwa pande zote husika,” alisema Dk Biteko.
Madai ya tegesha
Akizungumzia malipo ya fidia, Heche alisema hadi sasa, zaidi ya watu 5,273 kati ya watu 6,847 wanaotakiwa kuhama kupisha shughuli za uchimbaji madini wamenyimwa malipo ya fidia ya mali zao, wakidaiwa kuyategesha baada ya kupata taarifa za maeneo yao kuhitajiwa na mgodi.
Alisema hata hao wananchi zaidi ya 1,000 waliokubaliwa malipo ya fidia nao wana malalamiko ya ama kiwango cha fidia kuwa kidogo kulinganisha na thamani halisi ya mali au malipo yao kutoonekana katika kumbukumbu, huku wengine wakidaiwa kuwa tayari wamelipwa wakati wahusika bado hawajapokea fedha.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Michael Mtenjele alisema wanaobomolewa nyumba ni ambao tayari walilipwa fidia na kuwaomba wananchi waliopokea fidia kuondoa mali zao, ikiwemo nyumba, mbao, matofali, mabati kwa hiari badala ya kusubiri kubomolewa.
Chanzo - Mwananchi