DK.MPANGO AIAGIZA TFS KUPITIA UPYA UTARATIBU WA UTOAJI LESENI ZA UKATAJI MITI





Na Alex Sonna-DODOMA

MAKAMU wa Rais Dk.Philip Mpango, ameuagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kupitia upya utaratibu wa leseni za ukataji miti kwa ajili ya mkaa ili kuokoa maeneo ambayo yana uoto na vyanzo vya maji.

Dk.Mpango,ameyasema hayo jijini Dodoma  mara baada ya kumaliza kupanda mti katika shule ya msingi Msalato, tukio lililoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 59, ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika leo Januari 12,2023.

Amesema kuwa TFS lazima  mkapitie upya utaratibu huu wa utoaji wa leseni za ukataji miti kwa ajili ya mkaa kwani hivi sasa hali ni mbaya sana kama pale Mzakwe ambapo ndipo chanzo kikuu cha maji kwa jiji la Dodoma.

“Kila nikipita barabarani nasikitika sana unakuta misururu ya magunia ya mkaa na shughuli za ukataji miti zikiendelea sasa itafika wakati miti yote ikiisha kule mlimani ambapo ndiko eneo muhimu kwa ajili ya vyanzo vyetu vya maji vitakauka mara moja”amesema Dk. Mpango

Hata hivyo Dkt. Mpango amesema kwa sasa suala la upandaji miti linapaswa kuwa la lazima na kuziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafikia lengo la upandaji miti milioni moja na laki tano kwa mwaka kama ilivyopangwa.

”Ushirikishwaji wa sekta binafsi na wafanyabiashara katika upandaji na utunzaji miti pamoja na kuzisihi familia kuongeza juhudi katika upandaji miti na usafi wa mazingira. Pia amezitaka taasisi za serikali kupanda miti katika maeneo yao na kuhakikisha miti hiyo inaishi.”amesisitiza Dk.Mpango

Aidha  ameagiza Jiji la Dodoma kuratibu zoezi la usimamiaji miti iliopandwa ili kuhakikisha inaishi na kupendezesha jiji.

Dkt. Mpango ametoa wito kwa Waandishi wa Habari hapa nchini kutoa kipaumbele katika kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya upandaji miti na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.

”Ni muhimu kwa waandishi wa Habari kutoa habari za mifano ya wale walioweza kutunza mazingira ili wawe hamasa kwa watanzania wengine.”amesema Dk.Mpango

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema tayari mipango mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira imeanza kutekelezwa ikiwemo kugawa maeneo yaliopandwa miti  kwa taasisi za serikali na binafsi ili waweze kusimamia na kuhakikisha miti hiyo inaishi.

Waziri Jafo amemuhakikishia Makamu wa Rais zoezi la upandaji miti na kuitunza miti hiyo litakua endelevu wakati wote.

Naye Waziri Mkuu Mstaafu Mhe Mizengo Pinda ametoa wito kwa wananchi kuzingatia utaratibu wakati wa upandaji wa miti ikiwemo kuandaa mazingira ya upandaji na kufuata maelekezo ya wataalamu ili kufahamu aina ya mti na mahali unapopaswa kupandwa.

”Jiji la Dodoma linakabiliwa na upungufu wa mvua hivyo ni vyema uchimbaji wa mashimo pamoja na nafasi baina ya mti na mti ukawa wa kitaalamu zaidi ili kuepusha miti hiyo kutofikia lengo. ”ameeleza Mhe.Pinda

Awali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema upandaji miti katika vyanzo vya maji umepewa kipaumbele mkoani Dodoma kwa kuanza na Bonde la Mzakwe ambalo limekua na changamoto ya ukuaji wa miti.

Amesema tayari wataalamu wamewezesha aina ya miti inayopaswa kupanda pamoja na kuweka mazingira yatakayookoa miti hiyo dhidi ya hatari ya moto.

Previous Post Next Post