DKT. SAMIA AUANZA MWAKA NA WANASIASA

 


Ni mwanzo mpya? hili swali ambalo linagonga vichwa vya wadau wa siasa na wapenda demokrasia nchini wakati Rais Samia Suluhu Hassan akikutana na viongozi wa vyama vya siasa leo, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo unafanyika wakati kukiwa na vuguvugu la madai ya kuandikwa kwa Katiba mpya, kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi kabla ya mwaka 2024 na kuruhusu mikutano ya kisiasa.

Aina ya mkutano huu, ilishuhudiwa zaidi wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete na ikatoweka kipindi cha Dk John Magufuli, kuanzia Novemba 2015 alipofunga milango.


Ingawa Rais Samia alishakutana na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa jijini Dodoma Desemba 2021 katika mkutano wa vyama na wadau wa siasa, Chadema na NCCR-Mageuzi viliususia.

Huo ulikuwa mkutano wa kwanza tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 unaotajwa kugubikwa na ukiukwaji wa haki na sheria na kuacha majeraha kwa baadhi ya raia.

Mkutano huu wa leo utakuwa wa kwanza wenye sura ya kitaifa kama viongozi wakuu wote wa vyama vya upinzani hasa Chadema ambacho ndio chama kikuu cha upinzani kwa sasa.

Aprili 22 mwaka 2021 wakati Rais Samia akilihutubia Bunge aliahidi kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ili waweke mwelekeo wa kuendesha shughuli za kisiasa zenye tija na maslahi kwa Tanzania.

Hata hivyo, kukamatwa na hatimaye kushitakiwa kwa ugaidi kwa mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe kulionekana kuwa kikwazo cha mkutano huo, sasa kuna Moshi mweupe baada ya Mbowe kufutiwa mashitaka.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu inasema leo Rais Samia atakutana na kuzungumza na viongozi wa vyama vya siasa na mkutano huu unafanyika zikiwa zimepita siku mbili baada ya kuzungumza na Mbowe, mbele ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana.

Mazungumzo hayo na Mbowe yalifanyika wakati Rais alipopokea taarifa ya maridhiano baina ya CCM na Chadema yaliyodumu takriban miezi minane.


Wakati zuio hilo likiendelea, mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akiwa ziarani mkoani Mwanza alitangaza kuanzia Januari 5, wataanza kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima.

Rais Samia alipokea taarifa hiyo kutoka kwa Mbowe na Kinana na hiyo haikuwa mara ya kwanza viongozi hao kukutana tangu baadhi ya makada wa CCM akiwepo Nape Nnauye ambaye mwaka jana alikaririwa akisema mikutano hiyo ina afya kwa Taifa.

Nape alitoa kauli hiyo alipohojiwa katika kipindi cha Joto Kali la Asubuhi na ETv na kuzungumzia umuhimu wa mikutano ya hadhara akiifananisha na jicho la kuisaidia Serikali kujitizama.

Katika mahojiano hayo, Nape alisema anaamini mikutano hiyo ingeiimarisha CCM zaidi kuliko hali ilivyo sasa inapoongoza Serikali bila kuwa na mtu anayeisema hivyo ni rahisi viongozi kujisahau kwa sababu za kibinadamu.

“Mimi ni kati ya wale tunaoamini toka mwanzo kabisa, ni vyema tufungue watu wafanye siasa. Kama unataka kujipima, usijipime wakati mwenzako kafungwa mikono, nendeni mkashindane na kujenga hoja,” alinukuliwa Nape.

Mkutano huo wa Rais na viongozi wa vyama vya siasa unachukuliwa kwa umuhimu utakaotoa mwelekeo wa masuala hayo matatu ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wadau wa siasa na kuligawa Taifa.

Matamanio ya wanasiasa

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema Rais amefungua milango ya majadiliano na wao walishiriki kwa maslahi ya Taifa.

“Tumekuwa mstari wa mbele kuhimiza maridhiano ya kitaifa hivyo kikao cha kesho huenda ni mwendelezo wa hayo maridhiano yanayojengwa. Kuhusu ajenda atakuwa nayo aliyeitisha mkutano lakini kama itakuwa ni masuala ya Katiba mpya, mikutano ya hadhara na kupata tume huru ya uchaguzi tutakuwa mstari wa mbele kushiriki,” alisema.


Katibu Mkuu wa CUF, Hamad Masoud alisema huenda ripoti ya kikosi kazi ikawa ni miongoni mwa ajenda kwa sababu wadau wakubwa katika mchakato huo ni vyama vya siasa na si ajabu kwa sababu mwaka mpya umeanza.

“Tumepata mwaliko wa kikao hicho kitakachofanyika Januari 2 Dar es Salaam, kila chama kitatoa wawakilishi ambao ni mwenyekiti na makamu wake pamoja na makatibu wakuu wote wa vyama 19 vyenye usajili wa kudumu.

“Usikatae wito, kama katika maelezo yake (Rais) hatogusia suala la mikutano ya hadhara tutatafuta namna ya kumkumbusha. ‘‘Mikutano ya hadhara ni moja ya viungo muhimu katika demokrasia, huu ni mwaka wa saba haijafanyika, tuna matumani ataligusia, kama sivyo tutamweleza kwa lugha nzuri,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha DP, Abdul Mluya alisema wanategemea kusikia kanuni za mikutano ya hadhara zimeshakamilika kwa maagizo aliyoyatoa Rais kwenda kwa watendaji wake.

Pia, alisema wana matarajio zuio la mikutano ya hadhara litaondolewa na uelekeo mpya wa masuala ya demokrasia na utawala bora kuimarishwa hasa katika uchaguzi utakaofanyika siku za hivi usoni.

Naye, Katibu Mkuu wa Chama cha NRA, Hassan Kisbya alisema kitendo cha Rais Samia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kinazidi kujenga imani kwa Watanzania kuhusu dhamira yake aliyoianzisha kwamba bado inaendelea.

“Hatua hii inaonyesha dhamira ya Rais Samia kutaka kujenga Taifa lenye umoja na kufungua milango ya demokrasia haikuwa ya mashaka. Huu ni mwendelezo wake kwa yale aliyoyaahidi kwa wananchi,” alisema Kisbya.


Katibu wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Juma Ali Khatibu alisema “sijajua tulichoitiwa au tutakwenda kusikiliza ni nini, lakini ni wajibu wetu kuitikia na nina washauri viongozi wote wa vyama kuhudhuria. Mkubwa akikuita lazima uitikie wito na kumsikiliza.”

…anatimiza maneno yake

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema “tumepata huo wito lakini hatufahamu ajenda. Jambo muhimu kama ambavyo Rais ameahidi ni kufanya mashauriano na viongozi wa vyama vya siasa ili kuweka mazingira mazuri ya demokrasia nchini.”

Alisema Rais Samia anatembea katika maneno yake kwamba hilo ni jambo muhimu hasa katika wakati huu kwani alishaunda kikosi kazi kilichomaliza majukumu yake na juzi alipokea taarifa ya majadiliano kati ya CCM na Chadema, wadau muhimu kwa demokrasia ya Taifa hili.

“Michakato miwili iliyokuwa ikiendelea kwa wakati mmoja imemalizika, sasa ni wakati wa utekelezaji. Siku zote nasema nina imani kubwa na Rais Samia katika kujitoa kwake kwenye maridhiano na mageuzi yanayofanyika. Inawekezekana yanachukua muda mrefu kukamilika lakini ni kawaida mambo mazuri yanachukua muda mrefu, nina furaha sasa tunakutana viongozi wa vyama vya siasa, tutakachoelezwa tukipata nafasi ya kukizungumza, tutakieleza,” alisema Zitto.

Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Baraka Loshilaa na Bakari Kiango (Dar).

Previous Post Next Post