Miaka ya nyuma vijana wengi walikuwa wakiota kuzamia meli ili waende ughaibuni, wakiamini huko ndiko kuna maisha, hapa katikati mambo yakabadilika, ndoto nyingi za vijana zikawa ni kufanikiwa kimaisha kupitia biashara, kuajiriwa na shughuli nyingine za kiuchumi. Mambo ni tofauti kabisa kwa Eliud Mwakasege, kijana anayefanya vizuri kwenye fani ya vichekesho.
Elius, mzaliwa wa jijini Mbeya, wakati anakua ndoto yake kubwa ilikuwa kuja kuishi Dar es Salaam akiamini kuwepo jijini humo kutamwezesha kutimiza lengo lake la kuwa rubani.
Desemba 23 mwaka jana Eliud alitimiza mwaka mmoja wa kuishi jijini Dar es Salaam, aking’ara kupitia fani ya vichekesho na kuweka kando kabisa suala la urubani alilokuwa akilitamani utotoni.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Eliud anaeleza safari nzima ya maisha yake, changamoto alizopitia hadi kuibukia kwenye vichekesho kupitia jukwaa la Cheka Tu ambalo ndilo lilimwezesha kufungasha virago vyake kutoka Mbeya na kuhamia Dar na sababu za kuachana na ndoto ya urubani.
“Wakati nasoma nilitamani kuwa rubani na niliamini ili angalau niisogelee kazi hiyo lazima niishi Dar kwa kuwa ningeweza kuziona ndege mara kwa mara, halafu tukiwa huko mikoani tunaamini hapa ndiyo kitovu cha mafanikio,” anasema Eliud.
Mchekeshaji huyo anasema ndoto za urubani zilianza kuyeyuka baada ya kupata daraja la nne kwenye mtihani wa kidato cha nne.
“Nikiwa nimeshakata tamaa na kuamini kuwa maisha yangu sasa ni Mbeya na nitafute shughuli ya kufanya, kaka yangu mmoja alinipigia simu na kuniulizia nataka kusomea nini, sasa wakati huo simu janja ndiyo zilikuwa zinaingia, kuna mtu niliwahi kumsikia akisema ufundi wa simu itakuwa kazi yenye fedha nyingi, basi nikaropoka nataka kusomea mambo ya Tehama.
“Bila hiyana kaka yangu akaniambia nitafute chuo ili nisome, nikaitumia fursa hiyo kutafuta chuo jijini Dar,” anasema.
Anasema alipofika Dar alifikia kwa mjomba wake Temeke na kutafuta chuo na hatimaye akapata chuo cha Utumishi wa Umma, maarufu Magogoni, akijiunga ngazi ya cheti. “Nilifika chuoni mwaka ambao Elizabeth Michael, maarufu Lulu anasoma, yaani mtoto mzuri, nikasema eeeh hii bahati iliyoje nikazidi kuipenda Dar, basi nilikuwa nawahi chuo ili nimuone tu Lulu,” anasema.
Anasema hata hivyo maisha yake chuoni hapo hayakuwa kama ambavyo alitarajia, kwani licha ya kuwa mkubwa darasani alikuwa anashika mkia, jambo lililomuumiza kichwa na kumkatisha tamaa ya kutimiza lengo lake la kuwa mtaalamu wa simu.
“Hadi namaliza mambo yalikuwa hivyo, nilipata cheti lakini sikuona umuhimu wa kukichukua wakati sijui nitakifanyia nini, kwa mara nyingine ndoto za kuishi Dar zikayeyuka nikarudi Mbeya kwa wazazi wangu,” anasema.
Maisha mapya Mbeya
Anasema alirudi Mbeya lakini alikuwa akiumiza kichwa ataishije, kwani hana kazi zaidi ya kucheza kamari. “Nikiwa nimezama kwenye msongo wa mawazo, wakaja vijana walioanzisha kampuni ya kutoa huduma za burudani kwenye sherehe na kunitaka nijiunge nao kama mshereheshaji.
“Niliwaambia mimi sijawahi kufanya kazi hiyo na sijui chochote, wakaniambia nitaweza na wakaahidi kunielekeza baadhi ya vitu. Wakaniambia sura yangu inaendana na kazi hiyo, hivyo nitaifanya vizuri na kwa kunishawishi zaidi wakaniambia watanipangia chumba niishi mwenyewe. “Hapa kwenye chumba ndipo walipogusa hitaji la moyo wangu, sikutaka kujiuliza mara mbili, nikakubali na kumwambia mama kwamba nahama, alinishangaa, akasema unaenda kupanga ili iweje wakati najua utakuwa unashinda hapa kula, sikumsikiliza nikahama,” anasema.
Anasema aliamini kazi hiyo itakuwa mwanzo mpya wa maisha yake, hivyo alitafuta mbinu mbalimbali kuijua. “Nilikuwa ninakwenda nyumba za marafiki zangu kuangalia DVD za harusi na sherehe mbalimbali ili nijifunze washereheshaji wanavyofanya kazi, kabla sijaiva nikaambiwa kazi imepatikana.
“Zaidi ya kunilipia kodi ya miezi miwili katika chumba walichonitafutia pia walinipatia suti moja ambayo ilikuwa kitendea kazi kikubwa kwa MC, basi siku hiyo naambiwa kazi imepatikana natakiwa nikashereheshe kwenye harusi hata sijui nakwenda kusema nini. “Bahati nzuri yule mwenye harusi aliifanya kishkaji kwa kuwaalika rafiki zake na wengi nilikuwa nawafahamu, hivyo ilikuwa kama tunapiga stori, nilikuwa nawataja kwa majina fulani haya nenda katoe zawadi, kwa hiyo wengi walifurahia nikajikuta naanza kupata umaarufu eneo hilo, kazi zangu nyingi zikiwa vipaimara,” anasema huku anacheka. Hata hivyo kazi ziliadimika na kuishi kwa shida akiwa katika nyumba ya kupanga na hana mpango wa kurejea nyumbani kwao akiamini umri umekwenda. “Hapa niliamua kujiweka karibu na Mungu, ingawa huko nyuma mama alinishawishi bila mafanikio. “Kuokoka ni kama nilizidi kujipalia makaa ya moto, nilipitia maisha magumu wakati ule siwezi kusahau, yaani ilifika wakati nalala njaa, kuna siku nilitafuta Sh1,000 sikufanikiwa kuipata hata mama yangu nilimuomba akaniambia hana. Ilikuwa wakati wa majaribu kwangu maana nimeokoka, sitaki tena kujihusisha na wale vijana wenzangu niliokuwa nacheza nao kamari na sitaki hela zao halafu nina maisha magumu,” anasema.
Licha ya ugumu huo aliopitia hakufikiria kugeuka nyuma, aliendelea kuwa muumini mwaminifu kanisani na kuwa miongoni mwa vijana watiifu na vipenzi vya mchungaji. “Hatimaye nikapewa dhamana ya kuwa mchungaji wa vijana.
Alivyoingia kwenye vichekesho
Suala la uchekeshaji halikuwa kwenye kichwa cha Eliud na hakuwahi kufikiria kuna siku angeendesha maisha kupitia kazi hiyo.
Alijikuta upande huo kutokana na uwezo wake wa kuongea Kinyakyusa. Unaweza kujiuliza kivipi? Anasema pamoja na kuishi kwenye lindi la umaskini alijitahidi asikose simu janja na kifaa hicho ndicho kimemfanya kuwa miongoni mwa wachekeshaji wanaofuatiliwa zaidi mtandaoni.
“Nakumbuka siku moja nilikuwa na rafiki yangu nimemsindikiza kuosha bajaji yake, yule kijana aliyekuwa anaosha nilikuwa sijamuona siku nyingi nikawa namshangaa amenenepa akanijibu ameoa. Mazungumzo yale tulikuwa tunafanya Kinyakyusa... nikawa namwambia mwanamke bora ni anayejua kupika, nikapata wazo fasta....nikamwambia yule rafiki yangu arekodi video. “Ile video nikaiweka kwenye status yangu ya WhatsApp na Facebook, haikuchukua muda nikaona imesambaa kwenye makundi ya Wanyakyusa, nikawa napigiwa simu na watu kutoka mikoa mbalimbali, nikaona kumbe ni kitu kikubwa nikazitengeneza nyingi na huo ukawa mwanzo wa umaarufu wangu jijini Mbeya,” anasema.
Mwaka 2021 akapata taarifa za ujio wa Cheka Tu jijini Mbeya kwa ajili ya kusaka vipaji vya wachekeshaji. “Sikuwa nafahamu lolote kuhusu uchekeshaji, nilikutana na sauti nyingi zilizonishawishi kushiriki.” Hata mchungaji wake alimruhusu kushiriki shindano hilo na kumtia moyo akashindane na kushinda. “Maneno yale yalinitia moyo na kunifariji nikaenda kushiriki bila kujua ninakwenda kukutana na changamoto, akilini taarifa kuwa mshindi atakwenda Dar. “Nilifika na kukuta watu wengi wamejitokeza kushiriki, wakati wanagawa namba nikaomba niwe wa kwanza bila kujua nini hasa kinahitajika huko ndani, nilipofika pale nikaanza kusali na ndiyo ikawa kichekesho changu. Walishangaa nilichofanya na nilivyotoka nje nikajua ndio basi tena, lakini haikuwa hivyo nikachaguliwa kati ya waliofanya vizuri na hatimaye nikawakilisha mkoa wa Mbeya nikiwa na mwenzangu Neema,”anasema.
Kwa mara nyingine akapata fursa ya kwenda Dar safari hii akiwa chini ya jukwaa la kusaka vipaji vya uchekeshaji akichuana na wenziye kutoka mikoa mbalimbali. Kama ambavyo imekuwa ikimtokea huko nyuma alipofika kwenye jiji la ndoto zake, uwezo wake ulianza kushuka siku hadi siku na kuwa kwenye hatari ya kuondolewa kwenye shindano hilo. “Nikaanza kujiandaa kisaikolojia kurudi nyumbani Mbeya.
Anasema akiwa amekata tamaa akapata msaada kwa mmoja wa wachekeshaji ambaye pia anatokea Mbeya, aliyemfundisha kuandika miongozo ya vichekesho vya majukwaani. Msaada huo ulikuwa mkubwa kwa Eliud kwani wiki zilizofuata akaanza kufanya vizuri hadi kuingia kwenye fainali ambako aliibuka mshindi wa pili. “Ikawa ndiyo fursa ya kubaki Dar na kuingia kwenye orodha ya wachekeshaji wa Cheka Tu, jukwaa ambalo ninaendelea kufanya nalo kazi hadi sasa.
Hali yake ya mahusiano
Mchekeshaji huyu ameweka wazi kuwa yupo kwenye uhusiano ambao na ikipendeza Mungu anatarajia kufunga ndoa mwakani, akimwelezea mchumba wake kuwa anamtumikia Mungu kama ilivyo yeye. Anasema alimpeleka kanisa, ila sasa hivi yeye ndiye anamtumikia Mungu kumzidi. “Nakumbuka wakati nikiwa mchungani wa vijana nilikuwa napita kwenye eneo ambalo kulikuwa na duka lake nikatengeneza ukaribu naye aliponizoea nikamkaribisha kanisani kwetu ila alikataa. Anasema siku moja kukiwa na ugeni mzito wa askofu kanisani kwao, Eliud akiwa kwenye kamati ya maandalizi ghafla akamuona mwanamke huyo. “Alinieleza amekubali kuja kanisani na tangu wakati huo ukaribu wetu uliongezeka maradufu hadi kuanzisha uhusiano ambao unatarajia kutupeleka kwenye ndoa,”anasema.