Unaijua silika ya kunguru kunyea nguo nyeusi? Ni makusudi baada ya kujua kinyesi chake ni cheupe, akaona kuwa kunyea nguo nyeupe hakumpi kiki. Nia yake ilikuwa ni kumshughulisha mwenye nguo bila sababu. Akifanikiwa kwenye hilo ataanza kumchezesha kama kikaragosi; mara atarukia tawi hili na lile, atatambaa mchangani, basi tu ili mradi amkwaze.
Waswahili hawakukosea waliponena “penye mzoga ndipo nzi hukusanyika”. Kumbe lengo hasa la kunguru huyu ni michezo. Akiona watu ndipo naye anapotaka kuonekana. Kamwe hataanzisha ujinga wake iwapo hatamwona binadamu anayelinda nguo alizofua. Hii ina maana ukitaka asichafue nguo zako basi mpotezee. Akikuchokoza wewe ingia ndani ukalale, naye atajiondokea. Lakini kumbe sio kunguru pekee mwenye hulka za ajabu. Mtoto mchanga atatulia muda wote mpaka pale wageni wanapoingia nyumbani. Ataanzisha vurugu kama vile kumwaga soda ya mgeni, asipofanikiwa atavunja glasi na ukimzuia ataangua kilio. Akilia kwa muda mrefu mkampotezea atajinyea. Ili mradi tu mjue naye yupo.
Wakati mwingine fujo hizi hutokea kwa sababu ya kusaka fursa. Kunguru atakuchezesha ili ukose umakini, ampore mwanao kitumbua chake. Hata yule mtoto alimwaga kilio akijua wageni watambembeleza na soda zao. Kule mwituni utaona ndege wengi wakiandamana na wanyama wakubwa kama nyati na faru kwa sababu ya fursa ya kudonoa wadudu.
Jiji la Dar es Salaam, (enzi zake) lilifurika viumbe wa kila aina kwa sababu ya fursa. Kulikuwa na wakulima, wafanyakazi, wawindaji na wavuvi, ingawa maana halisi ya shughuli hizo haikuwa ile uliyoizoea. Hapa kuna wawindaji lakini si wa wanyama, bali wa mali za watu. Hata uchawi ulikuwa fursa. Kila kona ungepishana na matangazo ya “mganga wa majini”, “uganga wa kufuta madeni”, “mvuto kwa waume za watu” na kadhalika. Nadhani hii ndiyo sababu iliyowafurisha kila aina ya watu, wanyama, ndege, mijusi na wadudu. Ushawahi kuona mbwa anakula sembe kwa kisamvu? Basi hii ndio Dar.
Kila kiumbe alipata riziki kupitia kwa mwingine: Paka alipata kwa panya aliyeiba kwa mtu. Mjusi alidonoa wadudu, lakini akaishia kwenye mdomo wa bata aliyeishia kwenye domo la binadamu. Ukumbuke kuwa hapa ni binadamu pekee asiye na mipaka. Laiti Mwenyezi Mungu angelionyesha mambo yanayofanyika miilini mwa wanadamu… hakyanani hakuna ambaye angetembea hadharani.
Fikiria unapishana na muungwana mmoja kimyakimya, lakini kumbe anaendeshwa na injini kubwa zaidi ya meli ya uvuvi, anafua umeme zaidi ya radi na tumboni amebeba mashine ya kusaga iliyo kubwa kuliko ile ya Shirika la Usagaji. Fikiria tumboni kunasagwa sembe, makwasukwasu mpaka vingine hata mwenyewe havijui. Hujawahi kusikia mtu kakutwa na mawe tumboni?
Kichwa cha mtu huyu ni studio kubwa kuliko Rockfellers. Kina hekaheka zaidi ya baa ya uswahilini. Kichwani zinapigwa shangwe za Dulla Makabila, kuna mizozo ya baba mwenye nyumba na michepuko zaidi ya minane. Hapo sijamtaja mama mwenye jiko lake. Kuna kelele za watoto na hela ya shule, mwalimu wa twisheni na ada na kadhalika. Usisahau studio hii inatembea na biti zote hizo akipishana na honi za malori na matusi ya bodaboda waliomkosakosa.
Ndio nilikuwa nasema kwenye jiji kubwa kama hili, unaweza ukamsaidia mwizi wako kupakia mzigo aliokuibia bila mwenyewe kujua. Cha ajabu wezi wenyewe wamechanganyikiwa: Kuna mmoja aliiba kwenye ofisi ya watu halafu akasaini kitabu cha wageni na kuacha mawasiliano yake! Usidhani wanafanya kusudi, ni mambo yamesongana kutoka komweni hadi kisogoni, utosini hadi unyayoni!
Kwa taarifa yenu nimekuja Dodoma mara moja kusikilizia ishu fulani. Aise hongera kwa kila aliyeshiriki kuufanya Dodoma kuwa Mji Mkuu tangu enzi za Mwalimu. Bila shaka walijua matokeo yake yatakuwa ni haya tunayoyaona leo. Mji unapumua na bado unaita, yaani kama hii ndio Oman ya Afrika Mashariki. Vivutio vinapendeza, wenyeji wana afya, chakula kizuri… Akh msije sema kuwa nna mpango wa kuchumbia huku.
Jambo kubwa nililojifunza huku ni kuachiana nafasi. Yaani Wagogo wa sasa utadhani sio wabongo maana wana uono tofauti kabisa. Tangu unapouanza mji utaona nyumba zilizojengwa kwa tamthilia (ramani) ya kupendeza. Kila moja imekaa kwenye nafasi yake, sio kama kule kwetu nyumba ya tope inajengwa Uzunguni, halafu uswahilini ndio limesimama bangaloo. Bosi ataingizaje gari lake nyumbani wakati njia imezibwa na choo cha jirani?
Walioendelea majuu waliliona hili mapema, ndio mana mtaani kwao kuna kota hadi za kuku. Kila mtaa, nyumba inafikika.
Sisi hatuna budi kuanzia hapo. Bora kuanza upya kwenye uwanja mpya, kuliko unabomoa chumba ukibananishe na choo kwenye kijumba kilekile cha kale. Ukitanua wigo utaona hata akili za wanao zinaongezeka!