KASULU KUUKARIBISHA MWAKA KWA BONANZA JANUARI 7


NA RESPICE SWETU, MISALABA BLOG
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, inatarajia kufanya Bonanza la watumishi litakalohusisha michezo mbalimbali.

Akitoa taarifa ya Bonanza hilo afisa michezo wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Charles Mvuyekule amesema kuwa, Bonanza hilo litakalofanyika Januari 7 litahusisha michezo ya soka kwa wanaume, mpira wa pete, kuvuta kamba, kuruka, riadha na mbio.

Ameongeza kuwa, maandalizi ya Bonanza hilo litakalofanyika kwenye viwanja vya chuo cha ualimu Kasulu, yanaendelea vizuri na kuwaomba watumishi wa halmashauri hiyo kujiandaa kwa kufanya mazoezi yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu kwenye Bonanza hilo.

"Kupitia Bonanza hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Joseph Kashushura atazungumza na watumishi", amesema. 

Bonanza hilo litakaloambatana na chakula cha usiku, litakuwa la pili kufanyika katika historia ya halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kufuatia lililofanyika mwaka 2021.
Previous Post Next Post