KWA NINI RAHISI KUNUNULIWA POMBE KULIKO CHAKULA


 Una shida ya Sh50,000 ya haraka haraka, unachukua simu unampigia swahiba wako mmoja, “Muga eeh! Hebu naomba nisaidie Sh50,000 mara moja nitakurudishia kesho.”

“Dah! Ndugu yangu mbona mimi mwenyewe hali yangu mbaya,” swahiba yako anakujibu.

“Nisaidie ndugu yangu, au hata Sh20,000 tu, nimetoka na mtoto hospitali hapa kuna dawa nataka kumnunulia,” unatia mkazo ili aone ukubwa wa uhitaji wako.


“Kweli mzee, sina kitu, ningekusaidia,” anakwambia.

Basi unakubaliana na hali kwa sababu ukweli ni kwamba hujui mfuko wake. Hujui anasema uongo au ni kweli hana hiyo pesa, lakini wewe ni nani mpaka ujue hilo. Unakata simu, unampigia mtu mwingine.

Lakini baadaye, jioni, swahiba wako yule yule anakupigia simu, anakuuliza uko wapi?

“Nyumbani,” unamwambia.

“Niko Tuyajenge Bar hapa. Njoo chapchap kama vipi?” Anakuita.

Hapa Tuyajenge Bar ndipo mnapokunywaga pombe kila siku, lakini kwa sababu mchana ulimuomba akukopeshe Sh50,000, unakuwa njia panda, hujui anakuita kwa ajili ya pombe au kukupa ile Sh50,000.

Haraka unagundua majibu huwezi kuyapata ukiwa nyumbani. Unafunga safari mpaka Tuyajenge Bar, unafika unamkuta, na ile kukaa tu anaanza kukununulia pombe.

Unakunywa pombe, unakunywa pombe, unakunywa pombe mpaka basi. Halafu usiku kabisa mnaagana mkiwa mbwii na anakuacha bila hata senti kumi.

Ndiyo sasa unapata jibu kumbe alikuita kwa ajili ya kunywa pombe na wala hakuzingatia tatizo lako ulilomueleza mwanzo, lile la kuhitaji Sh50,000.

Unabaki unajiuliza sasa hiyo pesa aliyotumia kukunulia pombe si bora angekupa ili umnunulie dawa mtoto? Au sio?

Sasa sikia, kwanza kama unawaza hivyo utakuwa unayumba mno, unaanzaje kupanga matumizi kwenye hela ya mwanamume mwenzako? Hata kama ni kweli shida yako ilikuwa ni kubwa na msaada wake ungekuwa wa thamani sana, lakini pesa za mwanamume mwenzio hazikuhusu.


Lakini pia unadhani ni kwa nini Waswahili walisema mlevi yuko radhi akununulie pombe unywe mpaka ushindwe kutembea lakini sio kukununulia chakula hata kama una njaa ya kufa.

Hiyo ndiyo kawaida ya walevi. Jambo linalozua swali la kwa nini iko hivyo?

Ukweli ni kwamba, mlevi mwenzako anapokuita kukunulia sio hufanya hivyo kwa sababu anakupenda, bali anajifanyia yeye.

Mlevi mwenzako anakununulia pombe kwa sababu anapenda kampani yako. Na anagundua ili aipate, inabidi ailipie. Hawezi kuilipia kwa kukulipa pesa mkononi kama yuko kwa mangi ananunua sukari, badala yake anakulipa kwa kukulipia kile anachokipenda, kile kinachowakutanisha, pombe.

Kwa lugha nyepesi, hatilii maanani sana kuhusu maisha yako. Cha muhimu kwake ni kampani yako. Ni namna gani pombe zinanoga akiwa na wewe.

Previous Post Next Post