………………………..
Na Alex Sonna-DODOMA
MAMLAKA ya Udhibiti wa usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza nauli mpya za mabasi ya Mwendo kasi yanayofanya kazi zake jijini Dar es Salaam huku ikijiandaa kupanga nauli za treni ya mwendokasi (SGR)
Akitangaza nauli hizo mbele ya waandishi wa habari leo Januari 3,2022 ijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa (LATRA) CPA. Habibu Suluo amesema nauli hizo zimeongezeka kwa Sh100 kutoka nauli za zamani.
CPA Suluo amesema mabadiliko hayo ni kwa mujibu wa sheria na yamepitishwa na bodi ya Wakurugenzi baada ya kupokea maoni kuhusu nauli katika maeneo hayo.
Suluo amesema nauli ya mabasi ya Mwendokasi kwa njia kuu (truck route) ni Sh750 kutoka Sh600, njia ya mlisho (feeder router) ni Sh500 kutoka Sh400, njia ya mlisho na njia kuu (feeder +truck route) ni Sh900 kutoka 800 na njia ya kimara kwenda Kibaha ni Sh700 badala ya pendekezo la DART la Sh1,200.
“Mapendekezo haya ni kwa mujibu wa sheria lakini kama kuna mdau yeyote ana malalamiko au hakubaliani na haya alete malalamiko yake ndani ya siku 14 kutoka leo,” amesema CPA Suluo.
Kwa upande wa nauli za teksi mtandao zinazobeba abiria wanne nauli itakuwa Sh3,000 hadi 4,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama kuna safari nyingine toka hapo nauli itaongezeka kwa Sh800 hadi 1,000 kwa kilomita moja na safari inapokutana na vikwazo kama foleni nauli ya ziada itaongezeka kwa Sh80 hadi Sh100 nauli kwa dakika.
Pia, kwa upande wa magari yanayobeba abiria sita nauli elekezi ni Sh4,000 hadi Sh5,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama kutakuwa na safari ya ziada toka ya awali nauli itaongezeka kwa Sh1,000 hadi Sh1,200 kwa kilomita moja na vinapotokea vikwazo kama foleni nauli itaongezeka Sh80 hadi Sh150 kwa dakika.
Amesema kwa nauli za pikipiki ya kubeba abiria wawili nauli elekezi itakuwa Sh1,000 hadi Sh1,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama safari itaongezeka kutoka hapo nauli itaongezeka kwa Sh300 hadi Sh400 kwa kilomita moja na kama kutakuwa na vikwazo kama foleni nauli itaongezeka Sh50 hadi Sh70 kwa dakika.
“Kwa upande wa nauli za pikipiki mtandao zinazobeba abiria wasiozidi watatu ni nauli Sh2,000 hadi Sh2,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja na safari ya ziada itakayongezeka nauli itaongezeka kwa Sh500 hadi Sh600 kwa kilomita moja na kama kutakuwa na vikwazo njiani kama foleni nauli itaongezeka kwa Sh70 hadi Sh90 kwa dakika moja,” amesema CPA Suluo.
Aidha CPA Suluo Kuhusu usafiri wa mabasi amesema kuwa Mamlaka inawakumbusha mabasi yaendayo haraka kuzingatia kanuni ziliopangwa ili kufanya kazi kwa weledi.
CPA Suluo amesema bado wapo kwenye vikao vya masikilizano na wadau kuhusu nauli za treni ya mwendokasi (SGR) na bei kamili ya nauli hizo zitatangazwa mwezi ujao baada ya kuwasili kwa mabehewa nchini.