Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Mwanaume mmoja anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka
32, Daud John amekutwa akiwa amefariki chumbani kwake katika mtaa wa Kambarage
mjini Shinyanga.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Januari
2,2023 ambapo marehemu Daud John alikuwa ni mmoja wa wapangaji wa Nyumba ya
Mzee Hangwa katika mtaa wa Kambarage kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga.
Misalaba Blog imefika katika eneo la tukio na
kuzungumza na Mwenyekiti wa mtaa wa Kambarage Bwana Malick Juma Mbasha ambaye
ameeleza kuwa amepogea taarifa hizo leo asubuhi na kwamba baada ya kufikia
kwenye familia hiyo alipiga simu kituo cha polisi kutoa taarifa.
“Nilikuwa
ofisini kwangu asubuhi alikuja balozi wa nyumba kumi akasema kwenye nyumba ya mzee
Hangwa kuna kijana amekutwa amefariki basi tumefika kwenye tukio tukaambiwa
huyu kijana mara ya mwisho alionekana siku ya jana na alikuwa ndani analiza
mziki lakini asubuhi ya leo tumemkuta amefariki na mziki ukiendelea”.amesema
Mwenyekiti Malick Mbasha
Aidha Mwenyekiti huyo amewataka wananchi wa mtaa huo
ambao hawafahamiki kwenye ofisi ya serikali ya mtaa kupeleka taarifa zao sahihi
ili kuepusha changamoto pale zinapotokea.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo wakiwemo
wapangaji katika nyumba hiyo wamesema marehemu huyo hakuwa na tatizo lolote la
kiafya na kwamba baada ya kugundua kifo chake walikuta amefariki akiwa amelala
kitandani huku mziki ukiendelea kulia chumbani kwake.
Misalaba Blog pia imezungumza na Kamanda wa Jeshi la
Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi ambaye amedhibitisha
kifo cha Daud John.
Kamanda Magomi amesema jeshi la Polisi Mkoa wa
Shinyanga linaendelea na upelelezi ili kubaini chanzo cha kifo.
Marehemu Daud John alikuwa ni Mwenyekiti wa mafundi
wanaofanyakazi katika eneo la mnara wa Voda karibu na ofisi za CCM Wilaya ya
Shinyanga mjini.