Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amewataka vijana kujenga tabia ya kujitolea katika masuala ya kijamii kwa lengo la kusaidia wengine badala ya kusubiri kuajiriwa.Amesema kilio cha ukosefu wa ajira kwa vijana kitaondoka endapo kundi hilo litabadilisha mtazamo na kuanza kujitambua kwa kufanya shughuli mbalimbali zilizo kwenye mazingira yao kabla ya kufikiria kuajiriwa.
Katambi amewaeleza vijana kuwa Serikali inaendelea kutengeneza fursa mbali mbali za vijana kujikwamua kupitia mafunzo yanayotolewa na taasisi mbalimbali ikiwemo Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kinachotoa mafunzo ya huduma ya kwanza.
Naibu waziri huyo ameyasema hayo wakati wa kongamano la vijana lililofanyika katika chuo cha Ualimu Kigurunyembe jijini Morogoro chini ya uratibu wa tawi la Msalaba Mwekundu mkoani humo.
Amesema vijana wanapokuwa tayari kujitolea inawasaidia kupata uzoefu katika huduma au msaada wanaotoa na wanakuwa pia sehemu ya wanaoshiriki katika ujenzi wa uchumi wa taifa.
“Vijana mlio kwenye chama hiki mnafanya kazi kubwa ni wazi mna moyo wa kujitole naomba muendelee kufanya hivyo ili kuweza kusaidia nchi katika maeneo mbalimbali na kuwa nawahikikishia kuwa Serikali inaendelea kupambana kwa ajili yenu na watanzania wote kwa ujumla.
“Nikiwa kama kiongozi wa Serikali ninayesimamia eneo hili la vijana naahidi nataendelea kuzisimamia taasisi za umma zilizopo kwenye wizara yetu ili kutoa fursa kwa Chama cha Msalaba Mwekundu katika kutoa huduma ya kwanza huku wao wakibaki kama wasimamizi wa Sheria,” amesema Katambi
Awali Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu, David Kihenzile amepongeza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita zenye lengo la kuboresha maisha ya kila Mtanzania na kwamba Chama chake kama kisaidizi cha Serikali kwenye utoaji huduma za kibinadamu kwa umma wataendelea kutekeleza majukumu yao kama ilivyokusudiwa.
Kihenzile ambaye pia ni mbunge wa Mufindi Kusini amesema chama hicho kitaendelea kuwapika vijana kuwa tayari kujitolea na kusaidia pale utakapohitajika msaada wa kibinadamu.