NDOTO YA CHATO KUWA MKOA YAYEYUKA

 


Ndoto ya wananchi wa Wilaya ya Chato kuwa Mkoa imegonga mwamba baada ya mikoa jirani ya Kigoma, Kagera na Mwanza kutokuwa tayari kuachia maeneo yake ili kuunda mkoa mpya wa Chato.

Wazo la Wilaya ya Chato kuwa Mkoa liliibuka tangu enzi za utawala wa awamu ya tano ya Hayati Rais John Magufuli, hata hivyo limekuwa likijadiliwa katika ngazi mbalimbali kabla ya leo kukataliwa rasmi.

Akiwa wilayani Chato Oktoba 14, 2021 kwenye kilele cha mbio za Mwenge, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali inaangalia vigezo vitakavyo ruhusu Chato kuwa Mkoa.


“Bado Chato haijawa mkoa kuna vigezo kadhaa bado tunaviangalia vigezo hivi vikikidhi basi tunakwenda kulimaliza jaambo hilo,” alisema.

Hata hivyo, leo Januari 10, 2023 imeelezwa kuwa Chato haina vigezo vya kuwa mkoa.

Hayo yamebainishwa katika Kikao cha Ushauri wa Mkoa (RCC) wa Geita, wakati Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu wa Mkoa wa Geita, Frank Mashauri aliposoma majibu ya barua ya Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) yenye kumbukumbu namba CBD.132/503/01B/26 ya Oktoba 2022.

Akifafanua kuhusu kukwama huko, Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela amesema nia ya kuanzisha mkoa ilikuwepo na vikao vimefanyika na kupeleka mapendekezo kwenye mamlaka za juu.

Amesema Tamisemi imeandika barua kwenda kwenye mikoa jirani na mikoa hiyo imesema haipo tayari wilaya zake kwenda kuanzisha mkoa mpya wa Chato na kwa maana hiyo maombi ya Geita yamekataliwa.

“Mngeniambia mkoa ni kubwa tugawe inge- make sense (ingeeleweka), lakini mkoa huu haugawiki.

“Wakati mwingine unaweza kuwapa matumaini watu ambayo hayapo, sitaki kuwa muongo kuwapa watu matumaini ambayo hayapo nitakuwa mkuu wa mkoa wa ajabu sana,” amesema Shigela.

Shigela amesema akiwa mkuu wa Mkoa wa Tanga aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli alipinga masuala ya kugawa maeneo na hakuna mkoa wowote uliopendekeza kugawa maeneo yao na kuwataka viongozi kutojenga matumaini ambayo muda wake haujafika.


Amesema mkoa mwingine mkubwa ni Morogoro wenye halmashauri tisa kata 214 ukiwa na ukubwa wa eneo lenye urefu wa mita za mraba 73,039.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma aliwataka wadau kutumia busara kupatikana kwa mkoa mpya wa Chato kwa kuwa hata kupatikana kwa mkoa mpya wa Geita haikuwa rahisi na kwamba kilichopo sasa ni kupingana wenywewe kwa wenyewe.

“Tusishikane uchawi na tusikatishane tamaa kuwaliza mikoa haitakubali kwakuwa kuna rasilimali lakini kama kweli mkoa upo sisi Geita tumeshatoa mapendelkezo na Tamisemi wasitutege wakiona inapendeza wataugawa,” amesema Msukuma.

Kwa upande wake Mwenyekiti halmashauri ya Mbogwe, Vicent Busigwa amesema mvutano uliopo ni wa viongozi na sio wa wananchi.

Busigwa alisema Tamisemi ishauriwe kuliangalia upya jambo hili ili kupeleka huduma za wannachi karibu.

Naye Mbunge wa Mbogwe, Nicodemas Maganga, amesema, “Mwenyekiti Kanda hii ya Ziwa wananchi wote wanasubiri Chato kutangazwa kuwa mkoa na ukumbuke, Rais akizima mwenge Chato wananchi walikua wakisubiri mkoa kutangazwa jambo hili limekuwa siku nyingi.”



Chanzo - Mwananchi

Previous Post Next Post