Watu wawili wamefariki dunia Mkoa wa Arusha kwa matukio tofauti akiwemo askari polisi Stewart Kaino (47) kwa kuanguka akiwa nyumba ya kulala wageni.
Taarifa kwa umma, iliyotolewa leo Jumatano, Januari 11, 2023 na Kamanda wa Palisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo imesema Januari 8,2023 saa 08:30 usiku Jeshi la Polisi lilipokea taarifa ya uwepo wa mtu mmoja ambaye alifariki maeneo ya nyumba ya kulala wageni inayoitwa Mrina Shine iliyopo kata ya Levolosi jijini Arusha.
Kamanda Masejo amesema mara baada ya kupokea taarifa hiyo, Polisi walifika eneo hilo na kuukuta mwili wa Kaino ambaye ni Mkaguzi wa Polisi wa wilaya ya Arumeru.
"Bado tunaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira mazima ya kifo hiki na taarifa zitatolewa," alisema Kamanda Masejo.
Katika tukio jingine ni la Nelson Mollel (33), aliyefariki kwa kipigo ambaye anadaiwa alichapwa viboko zaidi ya 280 kwa tuhuma za kumtukana mama yake mzazi.
Alisema Mollel ambaye ni mfanyabiashara, mkazi wa kata ya Moivo, Wilaya ya Arumeru na Mkoa wa Arusha alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa.
Kamanda Masejo amebainisha uchunguzi wa awali wa Jeshi hilo umebaini Mollel alifariki dunia baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa na watu wanaodaiwa kuwa ni ndugu zake Januari 3, 2023 wakimtuhumu kumtukana mama yake mzazi (jina limehifadhiwa) na kumuibia.
"Baada ya kupigwa, ndugu hao waliendelea kukaa na majeruhi bila kumpeleka hospitali hadi Januari 8, 2023 alifikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru akiwa mahututi na kufariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
"Tunaendelea na upelelezi ili kuwakamata watu wote waliohusika katika tukio hilo ambao walikimbia baada ya kuona hali ya marehemu kuwa mbaya," alisema
Wazee wa jamii ya kimasai na Kimeru wilayani Arumeru mkoa Arusha, wamekuwa wakitoa adhabu ya kuwachapa viboko vijana ambao wamekuwa wakibainika kufanya matendo ambayo ni kinyume cha maadili.
Miongoni mwa matendo hayo ni kutukana wazazi, kunywa pombe mchana na kufanya vurugu, kuvaa nguo ambazo sio za heshima na kufanya uhalifu ikiwepo kupigana.
Mama mzazi wa marehemu Nelson, Janeth Kimario amesema kijana wake alimtukana Matusi ya nguoni Januari 1, 2023.
Amesema baada ya kutukwanwa ndipo alimwambia baba yake mdogo, Abel Mboya (45) ambaye alifanikiwa kumpata Nelson na kumpeleka porini na kuanza kumchapa fimbo akiwa na watu wengine.
“Lakini adhabu ilikuwa kubwa sana na ni kweli alistaili kuchapwa ila wamezidisha hadi nimempoteza mwanangu," amesema
Dada wa marehemu, Jackline Elias Mollel amesema mdogo wake amepigwa viboko 280 badala ya fimbo 70 vinavyopaswa kwa mujibu wa taratibu zao.
"Hii ni mila na desturi zetu, sisi wamasai lakini wamezidisha na pia wamemchapa kwa sifa sana, wamemvunja mbavu miguu na mikono," amesema
Polisi wilaya ya Arumeru wamethibitisha kupokea taarifa hizo hata hivyo, afisa mmoja wa polisi katika wilaya hiyo jina linahifadhiwa amesema msemaji ni kamanda wa polisi mkoa Arusha.
"Wewe unajua utaratibu, msemaji ni kamanda na nadhani mkimfuata atawapa taarifa rasmi ni kweli tukio hilo limeripotiwa," amesema
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha sheria na Haki za Binaadamu (LHRC), Arusha Wakili Hamis Mayombo alisema sheria ya kuchapwa viboko wakosaji inapaswa kukomeshwa kwani imekuwa na madhara kwa watuhumiwa lakini pia kuna vyombo vya kisheria vya kutoa adhabu.
"Hizo sheria za mila baadhi ni mbaya zinakiuka haki za binaadamu ni muhimu zikomeshwe," amesema