ROMBO KUTUMIA RISASI KUWAFUKUZA NYANI


Nyani ambao wamekuwa ni kero kwa muda mrefu katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wameanza kuondolewa kwenye makazi ya wananchi kwa kupigwa risasi baada ya jitihada za kuwafungia kengele na kuwawekea mitego kushindikana.
Nyani hao ambao wamekuwa wakitembea makundi kwa makundi wanadaiwa kuwa ni tishio katika wilaya hiyo kutokana na wingi wao, ambapo wamekuwa wakila mazao shambani, mifugo ikiwemo mbuzi, kuku na kuhatarisha usalama wa watoto.
Hali hiyo pia imesababisha baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo kushindwa kufanya shughuli za maendeleo na kulazimika kuyakimbia mashamba yao kutokana na nyani hao kula mazao yao kila mwaka na hawavuni chochote.
Akizungumzia leo Januari 8 katika operesheni ya kuwaondoa nyani hao, Mbunge wa Rombo ambaye ni Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuchukua hatua madhubuti ya kuwaondoa nyani hao, kwani wamekuwa ni kero ya muda mrefu.
"Kutokana na hali hiyo, tumekuwa tukitoa wito kwa mamlaka zetu kwamba hifadhi ziko kwa ajili ya watu na sio kwa ajili ya nyani, hivyo vikosi vipo mpakani mwa Rombo sasa hivi na nimeambiwa jana wameua nyani," amesema Profesa Mkenda

Amesema awali zilifanyika jitihada za kufunga nyani kengele, lakini walizoea zile kengele na hawakujali tena, kwa hiyo sasa hivi wanapigwa risasi ili kuwapunguza.


Amesema wananchi wa wilaya hiyo wataendelea kushirikiana na serikali katika kulinda Hifadhi za Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Ushiri Ikwiini, Alex Shayo amesema hatua ya kupunguza nyani hao kwa kuwaua itawezesha wananchi kufanya shughuli za maendeleo hasa kilimo.

"Idara ya Misitu ilileta mitego ya kisasa kutega hawa nyani katika kijiji cha Ushiri, lakini zaidi ya miezi miwili hawakuweza kutega nyani hata mmoja, kwa hiyo hatua hii ya kuamua kuwapunguza itarudisha imani kubwa kwa wananchi kwasababu ni tatizo," amesema. 

Previous Post Next Post