SABABU HASI ZA KUINGIA KATIKA UHUSIANO, NDOA

 


Watu wengi tumewaona kwenye ndoa wakiishi katika hali tofauti za maisha, wako wenye fedha na wasio nazo, wako wenye furaha na wasio nayo.

Yote hii huweza kuchangiwa na sababu nyingi, ikiwamo wanandoa hawa kujikuta wanaingia katika ndoa wakisukumwa na sababu zilizo mbovu na zisizo na msingi.

Ziko sababu njema na nzuri za ndoa zinazoongelewa sana na wengi maeneo mbalimbali.


Mimi nimejaribu kuzitafuta zile sababu zisizo nzuri ambazo wengine pasipokuwa makini wamezishikilia na kuziruhusu sababu hizi ziwasindikize katika ndoa na hivyo kujikuta wanajuta na kulia katika muda mwingi wa maisha baada ya uhusiano.

Hii pia ni sababu ya ukweli kwamba siku hizi idadi ya ndoa zinazovunjika ni kubwa sana kuliko awali.

Hali ya kiwango cha kudhamiria (commitment) kwa wanandoa ni kidogo sana na hivyo kushusha uthamani wa ndoa zenyewe.

Sababu hizi zitakuwezesha kuubadili mtazamo ulionao juu ya ndoa na kukusababisha kubadili namna unavyosema au kuwaza au kutenda kuhusiana na suala zima la ndoa na uhusiano.

Kuingia katika ndoa au uhusiano kwa lengo la kusaidiwa au kuongeza kiwango cha kiuchumi ulicho nacho.

Hapa wengine wamewageuza wapenzi wao kuwa mitaji au rasilimali ya kuwaondoa wao pamoja na ndugu zao kutoka kwenye umasikini.

Kwa kuthibitisha hili, wengine wamepewa majina kama buzi au ATM.

Katika penzi la namna hii hakuna mguso au muunganiko wa kihisia (intimacy) baina ya wapenzi, bali kinachowaunganisha pekee ni kile kilicho mfukoni au vile vinavyoshikika na kuonekana tu. Athari za penzi la aina hii linafungua milango mingi kwa wahusika kutokuwa waaminifu na hata kujihusisha na mapenzi nje ya uhusiano wao.

Hofu ya umri kupita na kuzeeka

Wako wengi sana, hususan wanawake ambao wamejikuta wakiwakubali wanaume wa aina yoyote ili mradi tu nao waolewe, maana umri wao ulionekana kusonga sana na hofu ya kutoolewa kutanda.


Mwanamume anayehusiana na mwanamke mwenye tabia hii huulizwa au kulazimishwa kila siku kwenda kujitambulisha kwa wazazi wa binti au kutangaza ndoa. Ndoa nyingi za aina hii zimeishia kwenye talaka na kutengana.

Wako wengine ambao kwa sababu wana kiu sana ya kupata watoto na wameogopeshwa sana habari kwamba wanaweza wasipate watoto kwa sababu ya umri wao, basi watacheka na kaka yeyote yule ilimradi tu waolewe au wazae naye. Wengine wa jinsi hii wamejuta sana baada ya kujikuta kuwa waliyezaa naye hakuwa baba bali mwanamume tu, tena kiruka njia, kwa hiyo wanawake hawa wameishia kulea mtoto au watoto wao wenyewe pasipo mzazi wa pili (single parenting), jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linawaathiri watoto wengi.

Kwa wale wanaokimbilia kuolewa ili wakazae watoto, kumbuka kuwa hata huko kwenye ndoa kuna waliokosa watoto.

Kuingia kwenye ndoa sababu ya mimba au mtoto aliyepatikana kabla ndoa.

Lazima kutofautisha kuwa sababu iliyowafanya kuzaa mtoto siyo itakayochochea kuoana.

Acha sababu ya kuoana kwenu iwe penzi lenu la dhati na sio mimba au mtoto.

Suala hili linahitaji pia wazazi wajue kitendo cha watoto kupeana mimba au kupata mtoto hakitoshi kuwa sababu ya kuwalazimisha kuoana, mara nyingi wazazi wamewalazimisha watoto wao kuingia katika ndoa kwa sababu ya mimba au mtoto na kujikuta wanawaharibia maisha yao mazima.

Ya nini kujiingiza katika uhusiano wa kudumu kisa umempa au umepewa mimba na kuifanya hiyo ndio sababu ya kulazimisha muishi pamoja kama mume na mke, wakati kabla ya mimba hiyo hakuna mmoja kati yenu aliyewahi kuwaza kuwa siku moja mtakuwa mume na mke, badala yake baada ya kipindi kifupi mnagundua kuwa hakuna penzi baina yenu, bali kinachowaunganisha ni mtoto pekee. Maumivu na vikwazo baina yenu vinawadhihirishia wazi kuwa ninyi wawili hamkutakiwa kuwa pamoja, bali mmelazimisha tu.


Kinachofuatia hapo ni kufungulia mlango penzi lingine nje au kufanya mkakati wa kusitisha uhusiano wenu ili kuitafuta furaha ya kweli sehemu nyingine.

Previous Post Next Post