Na Englibert Kayombo WAF – Dar Es Salaam.
Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema itaendelea kutoa kipaumbele na kuwalinda wazalishaji wa dawa na vifaa tiba waliopo hapa nchini ili kuongeza uzalishaji pamoja na ukuaji wa uchumi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo alipokutana na Wazalishaji na Wasambazaji wa Dawa na Vifaa tiba katika kikao cha pamoja Watendaji wa Serikali wakiwemo Bohari ya Dawa (MSD), Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar Es Salaam.
“Ni lazima tuangalie suala la kulinda viwanda vya ndani vya dawa na vifaatiba, hawa wamewekeza hata kama wanazalisha kidogo tunatakiwa kuwalinda kwa kutoa kipaumbele kwao kwenye ununuzi wa dawa na vifaatiba vya ndani ya nchi” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina thamini mchango wa Sekta binafsi kwenye kuwekeza katika maendeleo ya nchi hivyo uwepo wa Viwanda vinavyozalisha Dawa na Vifaatiba hapa nchini vina tija katika kuchochea ukuaji wa uchumi lakini pia uhakika wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa uhakika hapa hapa nchini.
Waziri Ummy amebainisha kuwa mpaka Mwezi Desemba 2022 kulikuwa na Viwanda 42 vya uzalishaji bidhaa za afya kati ya hivyo 18 vinazalisha Dawa (Viwanda 12 vya Dawa za Binadamu, 6 vya Dawa za Mifugo) huku Viwanda 24 vikijusisha na uzalishaji wa Vifaatiba.
Hata hivyo Waziri Ummy amevitaka Viwanda hivyo kuwa na mpango endelevu wa ukuzaji shughuli zao na kuendelea kuzalisha bidhaa za afya.
“Ni lazima mjipange, tusije tukaweka vikwazo kwa viwanda vya nje kuleta bidhaa hapa nchini ili hali hatuna uwezo wa kuzalisha za kumudu soko la hapa nchini hilo suala TMDA nawaachia mliangalie mtuletee majibu” amesisitiza Waziri Ummy Mwalimu.
Katika kikao hicho wazalishaji hao wa bidhaa za afya waliomba pia Serikali iangalie upya kodi ilizoziweka katika malighali zinazoingizwa nchini ili dawa na vifaatiba wanavyozalisha ziweze kutengenezwa kwa gharama ndogo na kumudu ushindani katika soko.
Waziri Ummy amesema kuwa amepokea maoni na ushauri kutoka kwa wazalishaji hao na kuahidi kuwa Wizara itajiridhisha na kwenda kufanya kikao na Hazina ili kuangalia upya gharama wanazotozwa wazalishaji hao kwenye kuingiza malighafi pamoja na vipuli vya mashine zinazotumika kutengeneza dawa na vifaatiba.
Awali akizungumza kwa niaba ya upande wa Wazalishaji na Wasambazaji bidhaa za afya, Bw. Fadhil Hezekia ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wafamasia ameiomba Serikali iweke mkazo zaidi katika kuongeza wanataaluma wa fani ya wafamasia dawa za viwandani ili kuwa na wazalishaji wengi wazawa wa hapa nchini.
Aidha Bw. Hezekea ameiomba Serikali ishirikiane zaidi na Sekta binfsi katika kutafuka masoko ya nje ya nchi ya Dawa na Vifaatiba ili kuongeza zaidi uzalishaji katika viwanda pamoja na ukuaji wa uchumi.