Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema mwisho wa mwezi huu Serikali inatarajia kutangaza bei mpya za vifurushi vya simu, ili kila Mtanzania amudu kuvitumia.
Kauli hiyo aliitoa , wakati wa uzinduzi wa mnara uliojengwa na mfuko wa mawasiliano kwa wote kwa kushirikiana na kampuni ya Vodacom, katika kijiji cha Kinenulo kilichopo kata ya Imalinyi, wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.
Alisema Serikali inakamilisha mapitio ili kuona namna ya kusaidia kupunguza gharama ili mwananchi wa kawaida apate huduma bila tatizo.
“Kwa kuzingatia hilo na ilani ya uchaguzi ya CCM, tumetakiwa kuwafikia zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, hivyo kujenga mnara pekee kama mtu hawezi kuutumia utakuwa hauna maana,” alisema.
Alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na kampuni za simu za mkononi inatafuta namna ya kuwapatia simu wananchi kwa mkopo ambapo watalipa kidogokidogo huku wakiendelea kutumia.
“Mtu wa kawaida kununua simu ya Sh300,000 ni ngumu kidogo, lakini tukimwambia weka elfu thelathini upewe simu ya laki tatu, atakuwa anakatwa kidogokidogo hata kama ni kwa mwaka mzima itawezekana,” alisema Nnauye.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba alisema Mkoa wa Njombe una jumla ya miradi ya ujenzi wa minara 32, ambapo 30 kati ya hiyo imekamilika na miwili ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ikigharimu Sh4.8 bilioni.
“Kazi zetu kubwa ni kuainisha sehemu zenye changamoto, baadaye kupeleka kwenye zabuni kwa ajili ya utekelezaji,” alisema Mashiba.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka aliipongeza UCSAF kwa namna ambavyo wamekuwa wadau wakubwa wa maendeleo kwenye sekta ya mawasiliano na Serikali, hususani kwenye maeneo ya vijijini.
Chanzo - Mwananchi