Vocha hizo sasa zinauzwa kwa bei ya juu kinyemela katika mikoa mbalimbali bila mamlaka husika kuzipandisha bei.
Kwa zaidi ya wiki moja sasa, vocha ya Sh500 inauzwa Sh550 au Sh600 na ile ya Sh1,000 inauzwa kati ya Sh 1,100 hadi Sh 1,200 katika mikoa mbalimbali ikiwamo ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Kilimanjaro ambako uchunguzi umefanyika.
Hata hivyo, Mwananchi lilizungumza na baadhi ya viongozi wa kampuni za simu ambao walikana kupandisha bei za vocha hizo.
Wakati kampuni hizo zikieleza hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabir Bakari alipozungumza na Mwananchi jana, alisema taarifa alizonazo hakuna vocha zilizopanda bei na kama zipo utakuwa ni utapeli huku akiwashauri wananchi kwa yeyote anayeuziwa kwa bei hizo atoe taarifa kituo cha polisi.
“Yaani umenunua vocha Sh1,200 halafu vocha yenyewe imeandikwa Sh1,000, sasa unalipaje fedha hiyo? Umefanya mawasiliano na mtandao husika na wamekuambiaje? Alihoji na kuongeza:
“Hakuna bei iliyopanda kama umepandishiwa nenda katika ofisi maalumu za Tigo au Voda ukaripoti au ukanunue kwenye maduka yao ya mawakala, kama vishoka wamekupiga nenda polisi, hakuna bei zilizopanda hata shilingi moja au senti tano,” alisema Dk Jabir.
Mkazi wa Songea mkoani Ruvuma, Stephen Mikael alisema tangu mwaka huu uanze ananunua vocha za kukwangua za Sh500 kwa Sh600 na ya Sh 1,000 kwa Sh1,200.
“Sasa hivi nimeacha kununua za kukwangua, nanunua kwa njia ya mtandao ingawa kuna makato kidogo,” alisema Mikael.
Mkazi wa Dar es Salaam ambaye hakutaja kutajwa jina alisema jana asubuhi alinunua vocha ya Sh500 kwa Sh550 na alipouliza sababu za kupanda ghafla, alijibiwa na muuzaji kwamba kwenye maduka ya jumla wanakonunua bidhaa hiyo imepanda.
“Baadhi ya mawakala wakubwa wameongeza bei, wamepunguza sehemu ya faida tuliyokuwa tunapata, lakini wametuelekeza tuendelee kuuza kwa bei iliyoandikwa kwenye vocha,” alisema.
Mmoja wa wafanyabiasha wa vocha wilayani Moshi, Jonas Mmbwambo alikiri vocha kupanda bei kwenye maduka ya jumla kutoka Sh 950 hadi 960, hali iliyoshusha faida waliyokuwa wakiipata.
“Hapa mjini bado tunauza bei ile ile iliyoandikwa kwenye vocha, lakini ukitoka nje ya mji kidogo na maeneo ya vijijini wao wanauza ile ya Sh1,000 kwa Sh 1,100 na ile ya Sh500 ni Sh 550,” alisema.
Mkurugenzi wa Biashara wa Vodacom Tanzania PLC, Linda Riwa alisema; “Vodacom hatujapandisha bei ya vocha, bado bei yetu ni ileile.
Hata hivyo, kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa vocha, walifanya marekebisho madogo ya kamisheni kwa asilimia 0.5 kwa wasambazaji wakubwa, ambao nao wamepunguza asilimia hiyo kwa wasambazaji wadogo wanaowauzia wateja na watumiaji wa vocha.
“Mfano vocha ya Sh500 ilikuwa ina kamisheni ya Sh30 na sasa imebadilika kidogo na kuwa Sh27.5.
“Inawezekana wauzaji wa kati na wa mwisho wanataka kutumia mabadiliko ya kamisheni ya Sh2.5 kupata faida zaidi kutoka kwa mtumiaji wa mwisho. Niwasihi hawa watu wasipandishe bei ya vocha kinyume na utaratibu,” alisema Riwa.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando alisema hakuna sehemu yoyote waliyoongeza bei za vocha tofauti na zilizotangazwa. Hata hivyo, alisema wanafuatilia suala hilo kwa ukaribu.
Imeandikwa na Bakari Kiango (Dar), Frola Temba (Moshi) na Damian Msyenene