Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), limesema wanafunzi 2,095 kati ya 2,180 waliofanya mtihani wa marudio wa darasa la saba uliofanyika kati ya Desemba 21 na 22 mwaka 2022 wamefaulu daraja A hadi C sawa na asilimia 96.1.
Limesema wanafunzi hao kati ya 2,194 waliofutiwa matokeo ya mtihani huo na Necta baada ya kubainika kufanya vitendo vya udanganyifu uliofanyika Oktoba 5, 6 mwaka 2022.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi amesema kati ya wanafunzi 2,194 waliofutiwa matokeo waliofanya mtihani 2,180, wachache hawakushiriki mchakato huo kwa sababu mbalimbali, akisema huenda wengine walikwenda nje ya nchi.
Amasi ameeleza hayo leo Jumatano Januari 4, 2023 wakati akitangaza matokeo ya upimaji wa darasa la nne na mtihani wa kidato cha pili uliofanyika kati ya Oktoba na Novemba 2022.
"Watoto hawa walisababishiwa kufanya vitendo vya udanganyifu, siyo kwamba hawana uwezo. Uwezo wanao tena mzuri lakini kwa sababu wanazozijua wenyewe wanawapa majibu ya mtihani na kuwaharibu watoto hawa.
"Wanawaondolea hali ya kujiamini katika jamii kwamba bila kupewa majibu hawafaulu wakati wana uwezo na mtihani huu wa marudio walioufanya wamesimamiwa na Necta na wamefanya vizuri na ufaulu mzuri," amesema Amasi.
Amasi amewataka watu wanaowapa majibu wanafunzi kuacha tabia hiyo, akisema wanaharibu Taifa na elimu kwa malengo binafsi sambamba na kuwaondolea hali ya kujiamini wanafunzi hao.
"Tuwaache watoto wafanye mtihani wenyewe na tuwafundishe vizuri ili waweze kufaulu, kama ambavyo umeona wamefanya vizuri bila usaidizi," amesema Amasi.
Kwa mujibu wa Amasi, matokeo ya wanafunzi hao yatawasilishwa katika mamlaka husika kwa ajili ya uteuzi wa shule za sekondari ili kuunga na wenzao katika hatua hiyo.
GUSA LINK HAPA CHINI KUTAZAMA MATOKEO
Chanzo - Mwananchi