Ticker

6/recent/ticker-posts

WANANCHI:HATUMTAKI DC KILOMBERO,MKURUGENZI MLIMBA

WANANCHI katika Wilaya ya Kilombero na Halmashauri ya Mlimba wamepaza sauti zao wakiwalalamikia viongozi wao wa wilaya na halmashauri hiyo kwa kile wanachosema kushindwa kuwasaidia katika changamoto mbalimbali zinazowakabili, hivyo kumuomba Waziri Mkuu na ikiwezekana Rais mwenyewe kufanya ziara kutembelea maeneo yao.
"Hatuoni ziara za viongozi katika kushughulikia kero zetu, lakini mbaya zaidi hata unapolalamika unaonekana mbaya, tunaomba sana Waziri Mkuu wetu Majaliwa Kassim Majaliwa aje mwenyewe katika Wilaya yetu ya Kilombero pia katika Halmashauri ya Mlimba na vijiji vyake, kuna mambo kadhaa hayako sawa," anasema Juliana Francis mkazi wa Kijiji cha Mofu, Halmashauri ya Mlimba.
Kwa miaka mingi, wananchi wanasema kumekuwa na ungezeko kubwa la wafugaji katika Bonde la Kilombero wakati inafahamika wazi kwamba eneo hilo ni oevu na halipaswi kutumika kwa shughuli za ufugaji.
"Tunafahamu eneo la Bonde la Kilombero ni oevu, lakini tunashangaa kuona mifugo ikiongezeka, mbaya zaidi mifugo inakula hadi mazao na tunapolalamika hatuoni hatua kali zinazochukuliwa. Tunafikiri uko umuhimu kwa Rais wetu kutuondolea viongozi wakuu wa wilaya na hata halmashauri ili kuleta wengine ambao watakuwa karibu na wananchi wote," anaongeza Mama Khaflan Mdenya.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Mlimba amekataa malalamiko hayo akisema ofisi yake inafanya kazi vizuri sana. Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi, Witness Kimoleta alisema anachofahamu kuna jitihada nyingi ambazo ofisi hiyo inafanya katika kusaidia jamii ikiwamo kushughulikia matatizo ya wananchi.
Mkuu wa wilaya wa Kilombero, Hanji Godigodi amekwenda mbali zaidi kusema kwamba ofisi yake imekuwa ikichukua hatua dhabiti katika kupambana na masuala mbalimbali ikiwamo migogoro ya wafugaji na wakulima.
"Tumezuia mifugo kuingia katika wilaya Kilombero" anasema mkuu huyuo wa wilaya.
Hata hivyo wananchi wanaendelea kuzilalamikia ofisi hizo wakisema hakuna ukaribu wa wananchi na ofisi ya halmashauri na wilaya huku migogoro baina ya wafugaji na wakulima ikilalamikiwa kwa miaka mingi kwamba hatua dhabiti hazichukuliwi kiasi cha kusababisha baadhi ya wananchi sasa kuanza kujichukulia hatua mkononi.

Post a Comment

0 Comments