" JUMUIYA YA WAZAZI WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAWAOMBA WANANCHI KUILINDA MIRADI YA MAENDELEO

JUMUIYA YA WAZAZI WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAWAOMBA WANANCHI KUILINDA MIRADI YA MAENDELEO

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Kmati ya utekelezaji Jumuiya ya wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini imewaomba wanachi kata ya Ngokolo kutoa taarifa za watu wanaoharibu miundombinu katika miradi mbalimbali maendeleo inayotekelezwa na serikali.

Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Bwana Fue Mrindoko wakati wa ziara ya kamati ya utekelezaji jumuiya hiyo baada ya kutembelea na kukagua uhai wa jumuiya ya wazazi kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga.

Mwenyekiti Bwana Fue amezungumzia miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba amepongeza usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo unaofanywa na viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuilinda miradi yote inayotekelezwa na serikali huku akisisitiza kutoa taarifa za watu wanaoharibu miundombinu ya miradi ili hatua stahiki zichukuliwe na mamlaka husika.

“Upo usimamizi mzuri ambao unasimamiwa na Manispaa chini ya uongozi wa Mkurugenzi wetu wa Manispaa ya Shinyanga ninachokiomba ni kwamba hii miradi inayojengwa na serikali ni miradi ya wananchi sisi wananchi tunatakiwa kuisimamia kwa sababu ni mali yetu kwahiyo tuungane kuilinda miradi yote”

“Suala hili la baadhi ya watu kuharibu miundombinu kwa sababu ni mali ya wananchi wote tuwe makini kuilinda miradi yetu, miundombinu yetu na kwa yeyote yule atakayeonekana ni chanzo cha kuharibu miundombinu yetu mara moja taarifa zitolewe kwa vyombo vya umma serikali na jeshi la polisi waweze kukamatwa ili wachukuliwe hatua zinazostahiki”.amesema Mwenyekiti Bwana Mrindoko

Kwa upande wake katibu wa Jumuiya ya wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Bi. Doris Kikabi ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kujenga madarasa na kuboresha mazingira ya wanafunzi shuleni ambapo amewasihi wazazi kusimamia na kufuatilia mienendo ya watoto wao ili waweze kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali.

Baadhi ya viongozi na wanachama wa jumuiya ya wazazi kata ya Ngokolo wameipongeza kamati hiyo huku wakiomba ziara hizo zifanyike mara kwa mara na kwamba hali hiyo itasaidia kuimarisha jumuiya za wazazi.

Kamati ya utekelezaji jumuiya ya wazazi leo Jumatatu Mei 15,2023 imeendelea na ziara zake za kutembelea na kukagua uhai wa jumuiya kwenye kata ambapo leo imetembelea jumuiya ya wazazi kata ya Ngokolo huku viongozi na wajumbe wa kamati hiyo wakitoa elimu mbalimbali ikiwemo masuala ya ukatili.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Bwana Fue Mrindoko akizungumza leo Mei 15,2023.

Katibu wa Jumuiya ya wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Bi. Doris Kikabi akizungumza na jumuiya ya wazazi kata ya Ngokolo leo Jumatatu Mei 15,2023.

Post a Comment

Previous Post Next Post