" MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YANAYOFANYA KAZI WILAYANI KASULU YATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE.

MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YANAYOFANYA KAZI WILAYANI KASULU YATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE.

Na Respice Swetu, Misalaba Blog.

Mkuu wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Kanali Isaac Mwakisu, amezitaka asasi na mashirika yasiyo ya kiserikali  yanayofanya kazi katika Wilaya ya Kasulu, kuyatekeleza majukumu yake.

Akifungua kikao kazi cha mwaka cha viongozi wa mashirika hayo kilichofanyika kwenye ukumbi wa boma mjini Kasulu amesema, kwa muda ambao amekuwepo katika Wilaya ya Kasulu, amebaini kuwepo kwa asasi na mashirika mengi ambapo kati yake, mengine hayafanyi kazi.

"Kuna mashirika mengi katika Wilaya ya Kasulu,  kinachofanyika hakilingani na wingi wa mashirika hayo na mimi niko tayari kubaki na mashirika machache yanayofanya kazi kuliko kuwa na wingi wa mashirika yasiyokuwa na kazi yoyote" amesema.

Akitoa mfano Kanali Mwakisu amelitaja shirika la Water Mission linalotoa huduma za upatikanaji wa maji kuwa miongoni mwa mashirika yanayofanya kazi vizuri.

"Water Mission wanafanya kazi nzuri sana, wamejenga miradi ya maji yenye thamani kubwa na kuondoa tatizo la maji kwa wananchi na mara nyingi wanakuja ofisini kunipa taarifa kuhusu miradi yao na kunichukua kwenda kuiona,  amesema.

Kufuatia hali hiyo, Mwakisu amewataka viongozi wa asasi na mashirika yasiyo ya kiserikali ambao hawajafika ofisini kwake, wafanye hivyo ili kumpa taarifa ya asasi zao, mahali walipo na aina ya shughuli wanazozitekeleza.

"Najua Watanzania tuko vizuri sana katika kuandika na kufanya michakato, mimi katika maisha yangu sijawahi kufundishwa kufanya michakato, nimefundishwa kufanya kazi na kutoa matokeo", amesema.

Ili kuhakikisha utendaji kazi wa mashirika na asasi hizo unakuwa endelevu, Mwakisu amewaelekeza pia viongozi hao kuweka mikakati ya kuziendesha taasisi hizo kwa kujitegemea badala ya kutegemea wafadhili.

Aidha alikitumia kikao hicho kukemea vitendo vya ushoga na usagaji na kuwataka washiriki wa kikao hicho kusaidiana na serikali kupiga vita suala hilo.

 "Watanzania tuna maadili na utamaduni wetu, na endapo nitagundua eneo lolote kwenye Wilaya yangu kuna viashiria vya kuwepo kwa jambo hilo hatua kali nitazichukua", ameonya Kanali Mwakisu.

Pamoja na kupokea taarifa za utendaji kazi za mashirika na asasi mbalimbali zilizopo wilayani Kasulu, kikao hicho pia kilipokea taarifa za miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye halmashauri pacha za Mji na Wilaya ya Kasulu zinazonufaika na mashirika hayo. 

Post a Comment

Previous Post Next Post