Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WATAALAM wa Ardhi na maafisa waandamizi wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma wataweka kambi katika Mtaa wa Ndachi uliopo Kata ya Mnadani
kusikiliza na kutatua migogoro ya Ardhi kwa siku 21 ili wananchi waweze
kuendeleza maeneo yao.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipofanya mkutano wa hadhara kusikiliza na
kutatua migogoro ya Ardhi kwa wananchi wa Mtaa wa Ndachi uliopo Kata ya Mnadani
jijini hapa.
Mafuru alisema kuwa Jiji la Dodoma limekuwa
likipokea malalamiko mengi sana ya Ardhi
kutoka kwa wananchi wa Ndachi ambayo yamekuwa yakipelekwa kwa namna
tofautitofauti. “Ndugu zangu wa Ndachi tumekuwa tukipokea malalamiko mengi
sana, kuna wanaokuja moja kwa moja ofisini, wanaotuma barua, wanaokwenda mkoani na Wizara ya Ardhi Mtumba.
Tutaweka kambi siku 21, naamini
tukikaa Ndachi kwa muda wa siku 21 hakuna kitu tutakiacha. Ndachi nitaweka
wataalam wanne ambao sio kutoka Ardhi,
wawili watakuwa wa sheria wengine watakuwa kutoka Maendeleo ya Jamii na
Mazingira. Naleta watu ambao sio maafisa wa ardhi ili wawe
‘neutral’ wasifanye kazi kwa kushawishiwa na wataalam wa Ardhi, tutafanya kazi kwa siku tano
halafu tutakutana kwaajili ya mkutano wa tathmini” alisema Mafuru.
Aidha, alielezea namna zoezi hilo la
kutatua migogoro ya Ardhi
Mtaa wa Ndachi linavyoenda kutekelezwa. “Tunamabalozi 86 na wanaaminika sana.
Mabalozi ndio wanajua watu wao wote, wanajua nani kahudumiwa na nani
hajahudumiwa, tunaenda kushirikiana nao watusaidie kumalizia hatua ya mwisho ya
ugawaji. Tutaanza na Mtaa wa Ndachi, tutagawa timu mbili, timu moja eneo
la Matuli na nyingine Ndachi. Tutakaa kwa siku tano, wenye changamoto kuanzia
leo mkajiorodheshe kwa mabalozi wenu ndani ya siku hizo njoo na lalamiko
lako lolote iwe mipaka, ‘invoice’, mapunjo ya asilimia za ugawanaji wa viwanja
njoo na kitu chochote usichoridhika nacho. Tutaenda kuongeza kasi ya utoaji wa
hati ndani ya hizo siku tano tukimaliza tutahamia Mtaa wa Mbwanga na Karume.
Akitoa malalamiko yake kwenye mkutano
huo mkazi wa Ndachi, Abilai Sharifu alisema “Mkurugenzi ondoa wote unda kamati
mpya kama kamati itaendelea kubaki na kuwa na watu walewale hatuwezi
kupata haki sababu kamati hiyo ndio wapigaji wakuu. Kwanza kwenye Kamati ya Ardhi kuna wengine wameingia wanasiku
20 tu, sisi ndio wanandachi hatuwezi kutatuliwa matatizo yetu na mtu asiye
mkazi wa Ndachi matatizo ya wananchi wa ndachi yatatatuliwa na mwanandachi. Ni
ombi langu Mkurugenzi uvunje kamati yote sababu hawajachaguliwa na wananchi wa
Ndachi.
Wakati huohuo Mkazi wa Matuli,
Mohamed Mamba alisema kuwa migogoro ya ardhi kwenye Mtaa wa Ndachi haiwezi
kuisha kama wananchi hawatashirikishwa katika kuunda kamati itakayosimamia
matatizo yao. “Ukitaka hii hali iishe kila sehemu ya mji wa Dodoma weka
kamati itakayochaguliwa na wananchi wenyewe wanaowaamini sio wanachaguliwa na
viongozi. Kamati ndizo zitashughulikia migogoro ya ardhi, unda kamati kila mtaa
watakayoikubali wananchi kwa idadi itakayotakiwa uitambue na mtaa uitambue
kamati hiyo ndio ipewe jukumu lakusimamia zoezi la ugawaji wa viwanja” alisema Mamba.
Post a Comment