Na Mapuli Misalaba
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Johari Samizi amepiga marufuku kufanyika Biashara ya chakula kwenye maeneo yote yanayozunguuka shule, ili kuwakinga wanafunzi na mazingira hatarishi ya kipindupindu.
Ameyasema hayo wakati akiongoza kikao cha kamati ya Afya ya msingi ya Wilaya ya Shinyanga ambapo amewataka wazazi na walezi kuchangia fedha kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi shuleni, ili kuwaepusha na mlipuko wa kipindupindu.
Amesema hatua hiyo ni tahadhari kabla ya madhara ambayo imelenga kuwakinga wanafunzi wote dhidi ya ugonjwa huo.
Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kuhakikisha wanakuwa na vyoo bora ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo hivyo ili kujikinga na ugonjwa wa Kipindupindu.
Aidha wagonjwa Nane wa kipindupindu kati ya tisa waliokuwa wamelazwa kwenye kambi maalumu ya kituo cha Afya cha Ihapa kata ya Old Shinyanga, Manispaa ya Shinyanga wameruhusiwa,huku mmoja akiendelea na matibabu.
Taarifa hiyo imetolewa na kaimu afisa Afya Manispaa ya Shinyanga Osward Ngulinga kwenye kikao cha kamati ya Afya ya msingi ya Wilaya ya Shinyanga ambapo ametaja mikakati mbalimbali inayoendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu ikiwemo utolewaji wa elimu katika jamii.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Dkt. Elisha Robert amesema wataalam wanaendelea kufanya juhudi mbalimbali kuhakikisha kipindupindu kinadhibitiwa.
Kwa upande wake mtaalam kutoka wizara ya Afya Suten Mwabulambo amesisitiza ushirikiano zaidi baina ya taasisi na wadau wote wanaohusika na mapambano dhidi ya kipindupindu.
Naye mstahiki meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuka amewakumbusha watumishi wa Halmashauri hiyo kuhusu umuhimu wa uwajibikaji kabla ya madhara hayajatokea.
Wajumbe wa kamati ya Afya ya msingi ya Wilaya ya Shinyanga wamesisitiza uchukuaji wa tahadhari dhidi ya kipindupindu ikiwemo uzingatiaji wa kanuni za afya.
Post a Comment