" KUWENI MABALOZI WA KUTETEA NA KULINDA MASLAHI YA MTUMIAJI WA HUDUMA YA NISHATI NA MAJI

KUWENI MABALOZI WA KUTETEA NA KULINDA MASLAHI YA MTUMIAJI WA HUDUMA YA NISHATI NA MAJI


Na Moshi Ndugulile

Wajumbe wa Baraza  na kamati za watumiaji wa huduma za nishati na maji EWURA CCC wametakiwa kuendelea kuwa mabalozi wa shughuli  zinazodhibitiwa na EWURA ili kulinda maslahi ya Wananchi

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA nchini katika hotuba yake iliyowasilishwa kwa niaba yake na Meneja wa EWURA kanda ya Mashariki Mhandisi Nyirabu Musira wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wajumbe wa kamati za watumiaji wa huduma za nishati na Maji za Mikoa yaliyofanyika Mjini Morogoro

Amesema wajibu mkubwa wa wajumbe hao ni kuhakikisha wanakuwa mabalozi wa huduma za nishati na Maji ambazo EWURA inadhibiti ili kuelewa nini anachopaswa kufanya mtoa huduma, ikiwa ni pamoja na kumwezesha mtumiaji kupata haki  na kutimiza wajibu wake.

“ukiona kituo cha mafuta ujue kinakuhusu,ukiona maji yanavuja  Barabarani ujue yanakuhusu,na ukiona umeme unakatikakatika na mgawo usioeleweka ujue unahusika,kimsingi wajumbe muanze ku-take interest kama mabalozi wa huduma za nishati na maji ambazo EWURA inadhibiti”

Amesema lengo la  kufanya hivyo ni kuhakikisha huduma za nishati na maji zinakuwa bora na endelevu.

Mkurugenzi huyo amewakumbusha wajumbe hao kusoma sheria,sera,kanuni na miongozo  inayosimamia huduma za nishati na Maji na kwamba wanapaswa kujielimisha  zaidi ili kuinua kiwango cha ufanisi katika utendaji kwa kushirikiana na serikali,watoa huduma na watumiaji wa huduma za nishati na Maji.

Amesisitiza kuendelea kwa ushirikiano utakaowezesha kuleta mabadiliko chanya katika utetezi wa haki na kusughulikia malalamiko na kero za wananchi kuhusu huduma za umeme,maji,mafuta na gesi za kupikia majumbani,ii kuimarisha huduma hizo kuanzia kizazi kilichopo na kijacho

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza Mhandisi David Ngula ameshukuru na kuipongeza EWURA kwa kuendelea kuliwezesha Baraza hilo kwa hali na mali katika utekelezaji wa mipango yake

Eng. Ngula amesema kamati za watumiaji wa huduma ya nishati na maji ni chombo madhubuti na muhimu kwa kuwa kimekuwa kikiwezesha  upatikanaji wa huduma bora na stahiki kwa watumiaji.

Katika taarifa yake aliyoiwasilisha kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa wajumbe wa kamati za watumiaji wa huduma za nishati na maji kaimu katibu mtendaji wa EWURA CCC Stella Lupimo amebainisha hatua mbali mbali zilizofikiwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha kamati 30 kwenye Mikoa 26 ya Tanzania bara.

Lupimo ameyataja mafanikio mengine kuwa ni kuwajengea uwezo wajumbe wa Baraza,watumishi na kamati za Mikoa,kufanya Mikutano ya Mwaka ya watumishi,kununua vitendea kazi,kufanikisha utatuzi wa malalamiko ya watumiaji,pamoja na kutoa msaada wa kisheria kwa walalamikaji ambao hawakuwa na uelewa wa kisheria.

Lupimo amesema ufinyu wa bajeti imesababisha kuwa na changamoto ya upungufu wa fedha hali inayochangia  kukwamisha utekelezaji wa baadhi ya majukumu

Amesisitiza zaidi wajumbe hao kuendelea kuwa kiungo thabiti baina ya watumiaji wa huduma ya nishati na maji,watoa huduma,Baraza na ewura ikiwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu kwenye hatua za kushughulikia malalamiko.

Amefafanua zaidi kuwa lengo la mafunzo hayo pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha Baraza linakuwa na wawakilishi wenye weledi na  kuwajengea uwezo washiriki hao ili kwenda kutekeleza jukumu la kutetea na kulinda maslahi ya mtumiaji huduma za nishati na maji  kwa ufanisi.

Amesema Mafunzo hayo yamefanyika baada ya kumalizika kwa muda wa wajumbe waliokuwepo Novemba 30,2023 na mchakato wa kuwapata wajumbe wapya kukamilika Disemba 2023, na kwamba wajumbe wapya watatumika  nafasi hizo kwa kipindi cha Miaka mitatu kuanzia  Januari 02,2024 hadi Januari Mosi,2027.

 Lupimo ameeleza kuwa Baraza limefikia maamuzi ya kutoa nafasi kwa wajumbe wa zamani likilenga kutumia ufanisi wa kiutendaji na uzoefu waliopata kwa kipindi chote cha utumishi wao kwenye kamati,lakini pia ni kutokana na utayari wao wa kuendelea kufanya kazi hiyo,na kwamba kuwa na mwendelezo wa kimajukumu ndani ya kamati za watumiaji.

Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za nishati na Maji  lina Jumla ya wajumbe 150 katika Mikoa 26 ya Tanzania bara 89 kati yao ni wapya huku 61 wanaendelea baada ya kufanyiwa tathimini na kukidhi vigezo vilivyokuwa vimewekwa.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post