Mganga mkuu wa serikali Prof. Tumaini Nagu, amewataka wananchi wa Wilaya ya Kishapu kuzingatia kanuni za afya ikiwemo matumizi ya vyoo, ili kuepuka magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu.
Profesa Nagu ametoa rai hiyo leo Jumanne Januari 23,2024 baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja katika vijiji mbalimbali vya kata za Idukilo na Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu, ambavyo vimeathiriwa na ugonjwa wa kuhara na kutapika.
“Kwa kweli tuzingatie usafi, usafi wa kila mtu binafsi lakini usafi wa mazingira yetu naomba la kwanza kubwa ni kunawa mikono wakati wote ukitaka kula, ukitoka chooni lakini hata ukimsafisha mtoto mdogo baada ya hapo unawe mikono kwa sababu vimelea hivi vya ugonjwa wa kipindupindu vinasambaa kwa haraka sana lakini pia hata tunapowahudumia wagonjwa kabla ya kuwapeleka kwenye vituo vyetu tuhakikishe kwamba tunanawa mikono kila wakati na kunawa mikono tunawe kwa maji safi na salama”.amesema Prof. Nagu
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amewataka viongozi wa wilaya ya Kishapu ikiwemo watendaji wa kata, kuhakikisha wanafanya msako kwenye kaya ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wale wote ambao hawazingatii kanuni za afya, ikiwemo kutokuwa vyoo.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa Mkoa, amesema watu 139 wameathirika na ugonjwa wa kipindupindu katika Mkoa wa Shinyanga ambapo kata ya Idukilo ni kata inayoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi na kwamba, jumla ya kaya 142 hazina vyoo kwenye kata hiyo.
“Kaya 142 kwenye kata hii ya Idukilo kukosa vyoo ni aibu inamaana wanajisaidia machakani na kipindi hiki cha mvua ukijisaidia machakani kile kinyesi chako kinaondoka na maji kinaenda mtoni kinaenda kwenye visima hapo unailaumu serikali hata choo chako unasubiri serikali ikujengee choo Idukilo ni Kishapu na Kishapu ni Shinyanga na Shinyanga ni Tanzania haipendezi”.
Watendaji wa kata kuanzia nikitoka hapa wale wote ambao hawana choo kuanzia leo pitisha msako asiyekuwa na choo alipe faini hana faini peleka Mahakamani na tusioneane aibu awe ni mtu maarufu asiwe maarufu, awe kiongozi asiwe kiongozi kamata huu ugonjwa siyo wa kuchekeana na ukimuona mwenzako anajisaidia kichakani wewe mwenyewe uwe chanzo cha taarifa toa taarifa sisi tumchukulie hatua".amesema RC Mndeme
Wakati huohuo, Mndeme ametembelea na kukagua miradi mbalimbali katika Wilaya hiyo ya kishapu, ikiwemo ujenzi wa madarasa katika shule ya Sekondari Mwadui Lohumbo, mradi wa maji Kishapu, chanzo cha maji kinachotumiwa na wananchi cha mto Tungu pamoja na kuzungumza na wananchi.
Mganga mkuu wa serikali
Prof. Tumaini Nagu akizungumza kwenye mkutano huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake
Wilaya ya Kishapu.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akipokea taarifa ya ujenzi wa shule kutoka kwa mkuu wa shule ya sekondari Mwadui Lohumbo Segeleti Masanja Machibya.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akitoa maelekezo kwa watekelezaji wa mradi huo katika shule ya sekondari Mwadui Lohumbo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akiwasisitiza wanafunzi wa shule ya sekondari Mwadui Lohumbo kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza malengo yao.
Mganga mkuu wa serikali Prof. Tumaini Nagu akizungumza kwenye mkutano huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake Wilaya ya Kishapu.
Mganga mkuu wa serikali Prof. Tumaini Nagu, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme na viongozi wengine wakiwa katika zoezi la msako wa kaya zinazotumia choo kata ya Idukilo Wilaya ya Kishapu.
Zoezi la msako wa kaya zinazotumia choo likiendelea katika kata ya Idukilo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
Zoezi la msako wa kaya zinazotumia choo likiendelea katika kata ya Idukilo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
Aidha katika ziara hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa polisi Janeth Magomi pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude.
Post a Comment