Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amesema
serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wanaowazuia watoto
wao kuripoti shuleni kwa ajili ya kuendelea na elimu ya sekondari hasa
wanaotarajiwa kuanza kidato cha kwanza Mwaka huu 2024.
Ameyasema hayo leo Jumatatu Januari 8,2024 wakati
akitembelea baadhi ya shule katika Manispaa ya Shinyanga kwa lengo la kukagua
zoezi la uandikishaji wa
wanafunzi wa elimu ya awali,Darasa la
kwanza na wale wanaoripoti kidato cha kwanza ambapo ziara hiyo ameambatana na
viongozi mbalimbali akiwemo mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi.
RC Mndeme amewataka wazazi na walezi kupeleka
watoto shule kwani serikali imeandaa
mazingira wezeshi ya walimu kufundisha
na wanafunzi kujifunzia sanjari na elimu kutolewa bila malipo huku akisema
hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaowaficha watoto wao.
“Watoto ni haki yao
kupata elimu niwaombe wale wazazi ambao bado hawajawapeleka watoto wawapeleke
shule nafasi bado zipo muda bado upo lakini kuanzia siku ya leo Tarehe 8
tunaanza masomo rasmi vi vyema sasa mtoto akaanza na wenzake kuanzia siku ya kwanza”
“Hawa watoto wanaoanza
na elimu bure tunawaambia wazazi wasahau suala la ada Dkt. Samia Suluhu Hassan amekwisha
lichukua, niwaombe tu wazazi wasiwaweke watoto nyumbani hasa wale wazazi ambao
wengine wanawatoto wenye ulemavu wasiwaweke nyumbani kwa sababu miundombinu
yote yakuwapokea watoto wenye ulemavu na wasiokuwa na ulemavu serikali
imeiandaa kwahiyo wazazi wawalete watoto wapate haki yao ya elimu”.amesema RC Mndeme
Aidha mkuu wa Mkoa huyo amewasisitiza wanafunzi kusoma kwa
bidii na kuepuka mambo yasiyofaa yanayoweza kukwamisha malengo yao katika elimu
ambapo amewahimiza kuwaheshimu walimu wao na kuzingatia mambo mazuri
wanayofundishwa shuleni hali ambayo itachangia pia kuwaepusha na mmomonyoko wa
madili.
Afisa Elimu
Mkoa wa Shinyanga Mwalimu Dafroza Ndalichako amesema maandalizi yote ya
kuwapokea wanafunzi wenye sifa za kuanza Mhula mpya wa Masomo kwa Mwaka 2024
yamekamilika.
Kwa upande
wao watoto walioanza Masomo leo wameipongeza serikali kwa kuwawekea miundo
mbinu rafiki ya kujifunzia huku wakiahidi kusoma kwa bidii.
Kwa upande wao walimu wakuu wa shule za Msingi na wakuu wa
sekondari wamesema mwitikio wa watoto wenye sifa za kuanza mhula wa masomo 2024
unaridhsha.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akikagua
zoezi la uandikishaji wa watoto katika shule ya awali na msingi Mwenge Manispaa
ya Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akikagua
zoezi la uandikishaji wa wanafunzi katika shule ya sekondari Ngokolo Manispaa
ya Shinyanga.
Post a Comment