Na Mapuli Misalaba,
Shinyanga
Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka
ya majisafi na usafi wa mazingira Shinyanga (SHUWASA) Mhandisi Yusuph Katopola amesema fedha zaidi
ya Milioni Mia saba zitatumika katika ujenzi wa mradi wa kuchakata majitaka ili
kufikia mita za ujazo mia moja (100) kwa siku ambapo mamlaka hiyo kwa sasa
inauwezo wa kutibu majitaka kwa mita za ujazo 40.
Ameyasema hayo wakati
akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo kwa waandishi wa
habari ambapo amesema kupitia mradi wa IFF – OBA, SHUWASA itatekeleza ujenzi wa
mradi wa kuchakata majitaka ikiwa lengo ni kufikia mita za ujazo mia moja na
kwamba mamlaka hiyo kwa sasa ipo kwenye hatua ya ununuzi wa Gari la majitaka
kama sehemu ya usimamizi wa mazingira.
Aidha Mkurugenzi mtendaji
wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola
amesema serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya fedha ilisaini mkataba wa fedha
na shirika la maendeleo la Ufaransa (French Development Agency – AFD) kwa ajili
ya ujenzi wa mradi wa majisafi na usafi wa mazingira kwa eneo linalohudumiwa na
SHUWASA.
Ameeleza kuwa mkataba huo
wenye thamani ya Euro Milioni 76 ni mkopo wa riba nafuu kutoka shirika la
maendeleo la Ufaransa na Euro ambapo Milioni moja zitatolewa na serikali ya
Tanzania na kwamba mkataba huo ulisainiwa Juni 20,2022 na unatarajiwa kuanza
rasmi Mwezi Mei Mwaka huu 2024 huku ukitarajiwa kukamilika Mwezi Mei Mwaka
2028.
Mhandisi Katopola amesema
SHUWASA inaendelea na utekelezaji wa mradi huo ambao unahusisha shughuli
mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mtandao wa majisafi kwa kilomita 298, ukarabati wa
mtandao chakavu wa maji safi kwa takribani kilomita mia moja (100) pamoja na
ujenzi wa matenki mawili ya kuhifadhi majisafi.
“SHUWASA tunaendelea na
utekelezaji wa mradi huu ambao unahusisha kazi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa
matenki mawili ya kuhifadhia majisafi yenye uwezo wa kuhifadhi mita mita za
ujazo Elfu moja mia tano (1,500) eneo la Kolandoto na mita za ujazo 250 eneo la
Didia, kuna kazi ya ujenzi wa mitambo minne ya kuchakata tope kinyesi eneo la
Ihapa na Mwagala kwa Manispaa ya Shinyanga lakini pia Kituli na Iselamagazi
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, kazi nyingine ni ukarabati wa mtambo wa
kutibu maji Ning’hwa na tathimini ya ufanisi na ukarabati wa bwawa la Ning’hwa,
lakini pia kuna kazi ya kuijengea uwezo taasisi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
jingo jipya la ofisi ya SHUWASA”.amesema Mhandisi Katopola.
“SHUWASA imeshatangaza zabuni
mbili za kupata wahandisi washauri kwa eneo la ujenzi na usimamizi (Design
& Supervision) pamoja na eneo la usaidizi kwa mamlaka (Technical
Assistance) kwa usimamizi wa mradi na zabuni moja ya kandarasi ya ujenzi
(Construction of portable water infrastructure) ambazo zipo katika hatua
mbalimbali za utekelezaji”.amesema Mkurugnzi mtendaji SHUWASA
Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira
Shinyanga (SHUWASA) amesema mamlaka hiyo
inaendelea na zoezi la kurasimisha maeneo mbalimbali ya mradi ambapo maombi ya
fedha za fidia kwa waathirika wa mradi yamewasilishwa Wizara ya Maji Oktoba 24,
2023 kwa ajili ya hatua zaidi za utekelezaji.
Amesema kwa sasa SHUWASA inaendelea na maandalizi ya nyaraka mbalimbali
kutoka kwa mfadhili na taasisi nyingine za serikali ili kuwezesha mikataba ya
shughuli za ujenzi kusainiwa na utekelezaji uweze kuanza.
Inatarajiwa kuwa mkandarasi atakabidhiwa eneo la mradi na kuanza
shughuli za ujenzi Mwezi Machi Mwaka huu 2024 ambapo mradi utahusisha ujenzi wa
vyoo vya kisasa katika maeneo ya kijamii ikiwemo shule, kituo cha afya pamoja
na stendi vipatavyo 36.
Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Shinyanga (SHUWASA) inajihusisha na utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na miji midogo ta Tinde, Didia na Iselamagazi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka
ya majisafi na usafi wa mazingira Shinyanga (SHUWASA) Mhandisi Yusuph Katopola na afisa mahusiano na mawasiliano SHUWASA Nsianel Gerald
wakiandika maswali mbalimbali yanayoulizwa na waandishi wa habari.
Post a Comment