" MHE. KATAMBI AOMBA USHIRIKIANO KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO

MHE. KATAMBI AOMBA USHIRIKIANO KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO

Na Suzy Butondo, Misalaba Media

Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini ambaye pia ni naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi  amewaomba viongozi wa CCM na serikali kushirikiane nae katika kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kutatua kero mbalimbali za wananchi  ili waweze kufanya  maendeleo  makubwa katika jimbo la Shinyanga.

Hayo ameyasema  wakati akizungumza  na wananchi wa jimbo la Shinyanga katika kata ya Kitangili, ambapo amesema ili kuweza kuijenga Shinyanga ni vizuri kuwa wamoja na kushirikiana katika kufanya kazi za maendeleo,  kuwahudumia wananchi na kuwaondolea manung"uniko .

Katambi amesema wananchi wanatarajia kuona maendeleo  makubwa katika maeneo yao, ambayo mengi tayari yamefanyiwa kazi,barabara zilikuwa hazipitiki madaraja yalikuwa hayapo, lakini kwa sasa barabara zinapitika, zahanati, mashule bado kero ndogo ndogo ambazo zinatakiwa kutatuliwa, ambapo ameahidi kuzifanyia kazi wakati wowote.

"Niwaombe wananchi muwaamini viongozi wenu kuanzia ngazi za mitaa,kata madiwani mbunge na Rais kwa kuwaletea miundombinu ya barabara zahanati, mashule na ninaamini tutaendelea kuboresha huduma mbalimbali za kijamii,"amesema Katambi.

"Leo naomba niwatajie michango mbalimbali nilioitoa katika jimbo langu kwa kipindi cha January hadi Murch 2024,kwa taasisi za dini na jamii, ikiwemo  kwenye Chama cha mapinduzi CCM na jumuiya zake .kwa ajili ya makongamano mabaraza na ugeni mbalimbali wa jumuiya zetu  jumla milioni 41.7"amesema Katambi.

Aidha amesema january hadi Decemba 2023 aliwawezesha wajasiliamali 910 kupata semina na kuwawezesha gharama za nauli na chakula jumla shilingi milioni 75, ikiwa ni pamoja na kuwezesha wajasiliamali na viongozi kupata semina ya matumizi ya majiko ya gesi na kugawa majiko ya gesi 1,680 pamoja na nauli jumla ya Shilingi milioni 92.4

“Jimbo langu linakata 17, ambapo kata zote tayari nimegawa fedha kutoka mfuko wa jimbo kwa ajili ya  kuchochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo 2024, kuboresha huduma zote za kijamii zikiwemo huduma mbalimbali za kijamii katika kata zote jumla Shilingi milioni 62.6”.

"Machungu yangu ni kuhakikisha kila mmoja tunaungana pamoja na kuhakikisha masikini anatendewa haki, tajili anatendewa haki, usaliti na roho mbaya sio mzuri tuungane kwa pamoja ili tuweze kuijenga Shinyanga yetu., mimi kazi yangu ni kufanya maendeleo, hivyo niwaombe viongozi wenzangu tuwatumikie wananchi wetu na tuhakikishe katika uchaguzi tunapata ushindi kwa kishindo"ameongeza Katambi.

Katambi  alimuomba Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi CCM  wilaya ya Shinyanga asimame imara  na kamati yake siasa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazohitajika kwenye jamii na kwuwataka madiwani  kusimamia miradi mbalimbali ya serikali inayoendelea kutekelezwa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Kitangili Mariam Nyangaka amesema yuko pamoja na mbunge katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika kata ya Kitangili kwani mpaka sasa kuna mabadiliko makubwa katika barabara na madaraja kulikuwa na shida kubwa lakini kwa sasa wananchi wana amani.

Baadhi ya wananchi wa kata ya Kitangili akiwemo Vedastina Nyakonga ameipongeza serikali pamoja na viongozi wa CCM kwa kusimamia vizuri na kuleta maendeleo ya barabara kwani ikinyesha mvua ilikuwa shida watoto kwenda shule kutokana na barabara kujaa maji lakini kwa sasa barabara zinapitika bila wasiwasi.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post