" MWANAUME MMOJA AUWAWA USIKU MANISPAA YA KAHAMA SHINYANGA, JESHI LA POLISI KUWASAKA WATUHUMIWA

MWANAUME MMOJA AUWAWA USIKU MANISPAA YA KAHAMA SHINYANGA, JESHI LA POLISI KUWASAKA WATUHUMIWA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaendelea kuwatafuta watu watatu wanaotuhumiwa kwa kosa la kumshambulia Seleman James Mabula, kwa kitu kizito kichwani hali iliyopelekea kifo chake.

Selemani James Mabula ni mwenye umri wa Miaka 50 mkazi wa kata ya Busoka Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga ameuwawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.

Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga tayari linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kuwabaini na kuwafikisha mahakani watuhumiwa waliohusika.

Misalaba Media imezungumza na kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi ambaye amesema tukio hilo limetokea majira ya saa saba kasorobo usiku wa kuamkia Machi 12 Mwaka huu 2024.

Kamanda Magomi amefafanua kuwa, watu hao walifika nyumbani kwa marehemu na kumtaka awapatie kile walichokuwa wakidai kuwa ni fedha zao, na baadae walianza kumshambulia kwa kitu kizito kichwani hali iliyosababisha kifo chake.

“Jeshi la Polisi tunaendelea kuwafuatilia waliohusika katika tukio la mtu anayejulikana kwa jina la Seleman James Mabula Mwenye Miaka 50 aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani karibu na Sikio la kulia na watu wasiojulikana”.

“Kilichotokea ni kwamba majira ya saa sita na dakika 45 usiku marehemu huyo akiwa amelala chumbani na mke wake walisikia Mbwa wanabweka nje Nyumba yao haina fensi lakini wanazizi la Ng’ombe kwahiyo mwanaume huyu baada ya kusikia Mbwa wanakweka akahisi kuna wezi wamekuja kuiba akatoka alipofungua tu mlango akakutana na watu  na maelezo haya ni kwa mujibu wa mke wake, watu hao walikuwa wamevaa zile kofia za kuficha uso”. “Alichokisikia mke wa marehemu alisikia sauti ya mmoja wa wale watu akimwambia tupe hela zetu wakati huo walikuwa wameshaingia naye ndani chumbani wakiwa wanamwambia tupe hela zetu mwanamke huyo alichokisikia marehemu aliuliza hela zipi mwamamke Yule alichosikia walimpiga na kitu kizito kichwani akadondoka na wale watu wakatokomea kusikojulikana’

“Marehemu huyo pia alikuwa katika Baraza la kata la Ardhi kwahiyo sisi tunaendelea na upelelezi ili tuweze kufahamu chanzo zaidi pengine tutaweza kufamamu kilichokuwa kikiendelea na tuweze kuwakamata hao watuhumiwa”.amesema SACP Magomi

SACP Magomi ametumia nafasi hiyo kuendelea kuwataka wananchi kuacha tabia za kujichukulia sharia mkononi huku akiwasisitiza watu wenye changamoto hizo kuziona mamlaka husika ikiwemo Mahakama ili kupata haki zao.

“Wito wangu ni kwamba kujichukulia sheria mkononi ni kosa na kwamba endapo tutawabaini kwa kweli sheria itachukua mkondo wake lakini niwaombe wananchi wa Mkoa wa Shinyanga ndani ya Halmashauri zote Kishapu, Msalala, Shinyanga vijijini na Kahama, Shinyanga mjini na Ushetu tuache kujichukulia sharia mkononi kwa sababu hata katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kila mtu anahaki ya kuishi lakini pia hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria kwamba wewe utoe uhai wa mtu mwingine, hivi sasa wale wote ambao watajichukulia sharia mkononi tutapambana nao kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake”.

“Kwahiyo niwaambie wananchi kama unachangamoto kama hii chombo cha Mahakama kipo na bahati nzuri zimeboreshwa kweli kweli na haki tunaziona zinatendeka wewe kama kweli unamdai mtu nenda Mahakamani fungua madai ili uweze kupata haki yako na siyo kuchukua sheria mkononi kwenda kwa mtu kumuua”.amesema SACP Magomi

Post a Comment

Previous Post Next Post