Na Mapuli Kitina Misalaba
Naibu Waziri ofisi ya Waziri mkuu kazi, vijana,
ajira na watu wenye ulemavu Mhe. Paschal Patrobas Katambi amewataka Wanawake
Nchini kuendelea kusimamia maadili mema kwa watoto ili wakue katika misingi
bora ya Taifa.
Ameyasema
hayo Mkoani Shinyanga kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani,
ambapo ametumia nafasi hiyo kuwasisitiza Wanawake wote kuendelea kushirikia na
Serikali katika kusimamia maadili mema kwa watoto ili kutengeneza vijana bora wenye kuchochea
maendeleo Nchini.
Mhe. Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Shinyanga mjini amesema ipo changamoto ya mmomonyoko wa maadili hasa kwa vijana
wa kike na wa kiume ambayo hupelekea vijana hao kufanya matendo yasiyofaa
ikiwemo uhalifu, wizi pamoja na ukatili na kwamba hatua hiyo hurudisha nyuma
maendeleo ya Taifa.
Amesema ni vema sasa jamii hasa Wanawake
kuwafundisha maadili mema watoto kuanzia ngazi ya Familia ili kuwaepusha na
mmomonyoko wa maadili huku akiviomba taasisi za Dini kuendelea kukemea suala
hili la mmomonyoko wa maadili na kwamba hatua hiyo itasaidia kila mmoja kuwa na
hofu ya Mungu wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.
“Ili tuwe na maadili ya Taifa lazima Mama zetu
ninyi muwe imara Mwanamke akiwa imara hata maadili tutayaona kuanzia ngazi ya
Familia tunachangamoto katika Taifa hili ya mmomonyoko wa maadili si kwa watoto
wa kike tu lakini pia hata wakiume tunaenda kuliua Taifa letu kwa sababu
tunaratajia kupata viongozi kutoka kwenye Familia zetu kwahiyo ni lazima
tusimamia maadili ya watoto wetu hasa watoto wa kike watoto wa kiume pia
tusiwasahau kwa sababu wengine wamekuwa wakiharibika kwa masuala ya ushoga,
madawa ya kulevya wanaharibika kwa kuwa na tabia mbaya, kufanya makosa ya jinai
yote haya yanaanzia kwenye ngazi ya kaya kwa sababu waharifu wengine ni wajomba
zetu, ndugu zetu wanatoka kwenye Familia zetu kwahiyo hapa katika kuangalia
uhalifu na maadili ya kitaifa ni lazima yaanzie kwenye ngazi ya kaya”.amesema
Mhe, Katambi
“Tuwafundishe
watoto wetu maadili mema ya utaifa, uzalendo lakini pia taasisi zetu za Dini
zitimize wajibu lazima tukemee matendo yaliyomabaya tukifuata misingi ya Dini
tutakuwa watu wema lakini pia tunao wajibu serikalini huku kwenye taasisi za
shule kote tunawajibu wa kulea maadili ya taifa hili ukiona leo kiongozi mla
rushwa mbadhirifu mwizi au hana mapenzi na Taifa lake inatokana na maadili na
ukimfuatilia zaidi utagundua alianza kuiba Kalamu shuleni au Madaftari kwa
wenzake”.amesema Mhe. Katambi
Aidha naibu Waziri Mhe. Paschal Patrobas Katambi amesema yapo mabadiliko mbalimbali ya kisera
yanaendelea kufanyika kwa lengo la kuimarisha usalama Nchini huku akiwataka
wanaume kutoingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi wa kike kwani ni
kosa kisheria ambao hupelekea kifungo cha Miaka 30 jela.
“Rais
Samia ametupa jukumu kubwa la kuhakikisha tunafanya mabadiliko makubwa ya
kisera ambayo yatasaidia kwenda kutunga sheria nzuri ambazo zitamsaidia
Mwanamke kumpa nafasi na fursa katika
uongozi lakini pia katika jamii na kupata fursa mbalimbali za ushiriki wake
katika ujenzi wa uchumi”.
“Na
tumefanya mabadiliko mengi hata kuangalia haki ya mtoto wa kike pamoja na
sheria ya Elimu ya Mwaka 2008 iliyofanyiwa marekebisho lengo ilikuwa ni
kumlinda mtoto wa kike dhidi ya unyanyasaji ugandamizaji na yote yale
manyanyaso ya kijinsia, hili ni pamoja na kuwapa haki yao ya elimu na ndiyo
maana hata unayeingia kwenye mahusiano na mtoto wa shule kuanzia shule ya
msingi mpaka kidato cha sita vyovyote
awe amekubali awe amekataa au kwa namna yoyote ukiwa na mahusiano naye ni sawa
na kosa la ubakaji na unafungwa Miaka 30 kwahiyo watoto wa kiume tukae mbali
kwenye jambo hili tuwaache watoto wetu wasome”.amesema
Mhe. Katambi
Naibu Waziri ofisi ya Waziri mkuu kazi, vijana,
ajira na watu wenye ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mhe.
Paschal Patrobas Katambi pamoja na mambo mengine leo baada ya kushiriki kilele
cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani amefanya ziara ya kutembelea na
kukagua shughuli za maendeleo kwenye kata mbalimbali za Jimbo la Shinyanga
ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto katika miundombinu ya Barabara, Elimu,
Umeme na Maji.
Naibu Waziri ofisi ya Waziri mkuu kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mhe. Paschal Patrobas Katambi akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Machi 8,2024.