SERIKALI INAENDELEA KUTAMBUA MCHANGO WA MWANAMKE NA KUTHAMINI JITIHADA ZAKE

 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa ushirikiano na Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam (DIT) kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani Machi 08.2024

  

Baadhi ya Washiriki wakimsikiliza Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (hayupo pichani),  wakati akifungua Kongamano la wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa ushirikiano na Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam (DIT) kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani Machi 08.2024

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imekuwa mstari wa mbele kutambua mchango wa mwanamke na kuthamini jitihada zake katika kuleta mafanikio na kuhamasisha mabadiliko ya jamii kwa kuzingatia usawa wa Jinsia.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa ushirikiano na Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam (DIT) kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani machi 08.2024

Dkt. Gwajima ameitaka  jamii kutumia makongamano  kama fursa  ya kuchochea wajibu wa wanawake kwenye maendeleo ya kiuchumi,Kijamii na kisiasa kitaifa na Kimataifa.

“Serikali kwa kushirikiana na Asasi mbalimbali imekuwa mstari wa mbele kuchochea harakati za kuimarisha, kutetea na kupigania maslahi ya wanawake kwa kuunganisha nguvu na sera kama familia moja.”amesema Dkt.Gwajima

Aidha amesema  Serikali inaendelea kutoa wito kwa jamii nzima kutambua kuwa ujenzi wa Taifa lolote Duniani hauwezekani isipokuwa kwa ushirikiano kati ya mwanamke na mwanamume.

“Ni ukweli usiopingika kuwa wanawake ni msingi wa mabadiliko mbalimbali ikiwemo masuala ya kiuchumi. Hivyo, wasipopewa fursa si rahisi kabisa kwa taifa kuendelea.”amesema

Hata hivyo ameisihi jamii kwa ujumla kushirikiana ili kuendelee kuongeza kasi ya uelewa wa masuala ya jinsia kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya ndani ya jamii na hatimaye kuongeza kasi ya maendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Dkt Bakari George  amesema, kupitia Kituo cha Kitaifa cha Utafiti na Machapisho Yahusuyo Wanawake (NWRDC) kwa miaka mitatu sasa imekuwa ikiandaa makongamano  ili kujadili tafiti na masuala kadhakuelekea siku ya wanawake duniani na mwaka huu wa imepata mshirika mwenza Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam ambapo Taasisi hizi zimeshirikiana kikamilifu kuandaa kongamano hilo.
“Kongamano hili linakusudia kujadili tafiti zipatazo 12 na maandiko ya mawazo bunifu manne (04) yaliyofanywa na wanataaluma na mashirika mbalimbali kuhusu masuala ya kijinsia”amesema  Dkt Bakari.

Amesema wana mipango ya baadaye ya Taasisi hizi kushirikiana kikamilifu katika kutatua changamoto za wanawake na jamii kwa ujumla ambapo Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru itatumia mbinu shirikishi kuibua changamoto za wanawake na kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam watatafuta suluhu za changamoto kwa kutumia teknolojia.

Naye Mwakilishi wa Taasisi ya teknolojia ya Dar es saalam (DIT),Dkt Daud Simbeye,amesema kuwa wataendelea kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii cha Tengeru ili kuhakikisha kuwa  tafiti mbalimbali zinafanyika  na kuweza kusaidia serikali kutunga sera na sheria zinazoweza Kuwainua wanawake  kiuchumi na katika fursa mbalimbali.
Awali  Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa DodomaBi.,Josephine  Mwaipopo ameshukuru taasisi hizo mbili kwa kuona Dodoma ni sehemu sahihi ya kufanyia Kongamano hilo kwani itakua ni chachu kwa wanawake wa Mkoa wa Dodoma kuamka na kujipambania kiuchumi na kuimarisha vipato vya  familia zao.
Previous Post Next Post