SHINYANGA YATEKELEZA MAAGIZO YA TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA, HATI SAFI ZAONGEZEKA WANACHAMA WAKIMIMINIKA KUSAJILIWA



Na, Ibrahim Mwakyoma - Misalaba Media

Mkoa wa Shinyanga umefanikiwa kutekeleza viapumbele saba vya tume ya maendeleo ya ushirika ambavyo vimewekwa na kamisheni ya tume hiyo kwa lengo la kuhakikisha ushirika unaendeshwa katika hali ya kisasa zaidi.

Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Shinyanga Bi.Hilda Boniface  amebainisha hayo wakati akizungumza katika siku ya kwanza ya jukwaa la Maendeleo ya Ushirika mkoa wa Shinyanga linalofanyika kwa siku mbili kati ya Machi 21-22 katika Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi,Taasisi ya Elimu ya  biashara Kizumbi Manispaa ya Shinyanga na kuvielezea vipaumbele hivyo kuwa ni uwekezaji katika mifumo ya kidigitali.

Aidha amevitaja vipaumbele vingine kuwa ni pamoja na kuharakisha mchakato wa uanzishwaji wa benki ya maendeleo ya ushirika,uboreshaji wa sera na sheria  za usimamizi wa vyama vya ushirika,uhamasishaji wa ushirika katika makundi maalum,uimarishaji na uthamini wa mali za vyama vya ushirika na kushirikiana na wadau mbalimbali katika uendeshaji wa sekta ya ushirika.

“Nikiri kabisa wazi kwamba tunaipongeza tume ya maendeleo ya ushirika kwa kuleta mfumo wa usimamizi wa vyama vya ushirika, umeturahisishia kazi kwa maana ya usimamizi ilikuwa ili mtu alete mkataba wake basi lazima muonane uso kwa uso’kwa hiyo unapunguza urasimu,uonevu na mambo mengine,sasa hivi mikataba,makisio na nyaraka zote vinapita kwenye mfumo wa usimamizi wa vyama vya ushirika kuja kwa mrajis kwaajili ya kupata idhini kwahiyo tunampongeza mrajis wetu wa vyama vya ushirika kamisheni ya tume ya maendeleo ya ushirika kwa hii kazi kubwa ambayo ameifanya ya kusimamia ushirika na kuleta mageuzi makubwa ya ushirika katika nchi yetu na sisi wanashinyanga tunaemedelea kuyaona matunda hayo”amesema Bi.Hilda.

Akielezea hali ya usajili wa wananchama katika mfumo wa MUVU amebainisha kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2023 wakulima na wanachama 15400 walisajiliwa na hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2024 kumekuwa na ongezeko kubwa ambapo jumla ya wakulima na wanachama zaidi ya 72000 kutoka katika vyama 273 vya ushirika na mikataba zaidi ya 40 ya vyama imepita katika mfumo huo.

Akizungumza kuhusiana na ukaguzi uliofanyika kati ya Julai 2023 hadi Februari 2024 ndani ya vyama vya ushirikia katika mkoa wa Shinyanga,Mkaguzi wa vyama vya ushirika mkoa wa Shinyanga kutoka shirika la ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika Bw.Rodrick Kilemile amesema kwamba ukaguzi ulifanyika katika vyama 149 na kati ya  hivyo 46 vilipata hati safi ikiwa ni ongezeko la hati 39, 77 vilipata hati yenye mashaka 22 vikipata hati zisizo na maoni,na vyama vinne vilipata hati mbaya.

Mgeni rasmi katika jukwaa hilo ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti na mafunzo kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Bw. Juma Mokili Juma aliyemuwakilisha mrajis wa vyama vya Ushirika Tanzania amevitaka vyama vya ushirika kuendelea kuzingatia sheria kanuni na miongozo ya vyama vya ushirika.

“Mrajis mkuu ameniagiza nije kuwapa pongezi kwa kuchangia mtaji wa kuanzisha benki ya taifa ya ushirika,tunayo taarifa kuwa kufikia jana (Machi 20) zaidi ya milioni 153 kwenye mtaji wa kuanzisha benki yetu ya taifa zimetoka mkoa wa Shinyanga,sasa mrajis wa vyama vya ushirika agizo lake anawataka wale wote ambao hatujafanya hivyo tufanye bila kusita na wale ambao tayari tumeshachangia ikiwa ni mwanachama mmoja mmoja ama mkulima mmoja mmoja lakini ikiwa ni chama cha ushirika tuweze kuongeza hisa zetu maana ni uwekezaji usio na shaka lolote”amesema Bw.Juma

Katika hatua nyingine ameupongeza uongozi wa vyama vya Shirika mkoa wa Shinyanga chini ya Mrajisi msaidizi kwa uandikishaji wa wanachama wengi kwa mfumo wa kidigitali wa MUVU ambapo hadi sasa wananchama wapatao 720,122 wameandikishwa na kueleza kwamba Shinyanga ni mkoa  wa tatu kitaifa kati ya mikoa   iliyofanya vizuri katika eneo hilo.

Mgeni rasmi katika jukwaa hilo ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti na mafunzo kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Bw. Juma Mokili akizungumza.

Previous Post Next Post