HIZI ndio zetu, hizi ndio shoo za Chama. Kisasi ni haki. Unyama ni mwingi sama. Ndivyo walivyokuwa wakitamba mashabiki wa Simba baada ya timu hiyo ya Msimbazi kutinga hatua ya robo fainali ya CAF kwa mara ya tano katika miaka sita kwa kuichakaza Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa mabao 6-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Hesabu sasa ni kujua nani watakutana naye katika mechi za mtoano baada ya Wekundu hao kuungana na mahasimu wao Yanga kuandika historia ya kuingiza timu mbili kwa mkupuo katika robo fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi ya ngazi ya klabu Afrika kwa mara ya kwanza.
Yanga ilitangulia mapema ikiwa na mechi mkononi baada ya kuifunga CR Belouizdad ya Algeria mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Februari 24 kabla ya juzi kumalizia mechi ya kukamilisha ratiba kwa kichapo cha 1-0 ugenini dhidi ya mabingwa mara 11 wa michuano hiyo, Al Ahly huko Misri.
Straika Fiston Mayele aliifuingia timu yake ya Pyramids ya Misri mabao yote mawili katika sare ya 2-2 dhidi ya FC Nouadhibou ya Mauritania lakini timu yake ilishaaga mapema michuano ikimaliza mkiani mwa msimamo wa Kundi A, ambalo limeongozwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyomaliza na pointi 13 baada ya jana kuifunga TP Mazembe 1-0 kwa penalti ya Peter Shalulile. Mazembe imemaliza ya pili kwa pointi 10.
Mechi ya jana iliyopewa jina la ‘Vita ya Kisasi’ ilikuwa tamu sana kwa Wanamsimbazi ambao waliingia uwanjani Kwa Mkapa wakikumbuka kichapo cha 3-1 kutoka kwa wababe hao wa Botswana cha Oktoba 24, 2021 uwanjani hapo kilichoing’oa Simba kwa sheria ya mabao mengi ya ugenini baada ya Wekundu kushinda 2-0 ugenini katika mechi yao ya kwanza ya hatua ya pili ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mwamba wa Lusaka ‘Triple C’ alileta takribani matatizo yote yaliyotokea langoni mwa Jwaneng.
Alitoa asisti ya bao la kwanza la Par Omar Jobe, akatoa na asisti ya bao la pili la Saido Ntibazonkiza, akatengeneza bao la tatu la Kibu Denis ‘Mkandaji’, akafunga mwenyewe bao la nne, alikuwepo katika eneo la tukio la bao la tano lililofungwa Ladack Chasambi na akaanzisha kona fupi kwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyetoa asisti ya bao la sita lililowekwa kambani kwa kichwa na kiungo wa boli Fabrice Ngoma. Kilikuwa kipigo cha kuumiza sana kwa wageni na kitamu sana na kukumbukwa kwa wenyeji. Na ni jinamizi ambalo litabaki kuwatokea Jwaneng kwa miaka yote ya maisha yao, Simba ikiingia robo fainali ya tano ya CAF katika miaka sita -- nne zikiwa za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shiriksho Afrika.
Katika droo ya robo fainali, kwa kumaliza katika nafasi ya pili ya kundi B ikiwa na pointi 9, nyuma ya Asec yenye pointi 11, Simba inaweza kukutana na Mamelodi Sundowns, Al Ahly au timu iliyomaliza kileleni mwa kundi C kati ya Petro Atletico na Esperance zilizocheza mechi zao baadaye jana usiku.
Yanga pia itakutana na timu moja kati ya Mamelodi, Asec na kinara wa Kundi C katika mechi za robo fainali.
Simba iliingia na mpango wa kuumaliza mchezo katika kipindi cha kwanza ili isiwe na presha kipindi cha pili na katika hilo ilifanikiwa kutokana na idadi ya mabao (3) ambayo iliyapata ndani ya dakika 15.
Simba ilifunga bao la kwanza dakika ya 7 ya mchezo kupitia Sadio baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Clatous Chama, bao la pili lilifungwa na Mgambia, Pa Omar Jobe dakika ya 14 huku astisti akitoa Sadio na chuma ya tatu ikafungwa na Kibu Dennis dakika ya 22.
Vijana hao wa Abdelhak Benchikha walionekana kulisakama lango la Galaxy huku wakishambulia zaidi kupitia upande wa kushoto ambako alikuwa akicheza, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Chama ambaye muda mwingine alikuwa akipishana na Sadio aliyekuwa akicheza nyuma ya mshambuliaji ya mwisho, Jobe.
Ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza Simba ilifika mara 13 kwenye eneo la hatari la Jwaneng hiyo ishara tosha kwamba safu yao ya ushambuliaji iliyonogeshwa na Sadio na Chama ilikuwa na uchu wa mabao.
Mabao yote ambayo Simba imefunga katika kipindi cha pili ilikuwa ndani ya 18 lakini pia utulivu wa viungo wao wa kati, Fabrice Ngoma na Babacar Sarr uliifanya timu hiyo kuwa bora eneo la kati huku Hennock Inonga na Che Malone wakiwa kikwazo kwa washambuliaji wa Galaxy.
Njaa ya mabao kwa Simba ni kama ilipungua katika kipindi cha pili ndipo kocha Abdelhack Benchikha alipoamua kufanya mabadiliko kwa kumtoa Sarr na kuingia Mzamiru Yassin ili kuongeza nguvu ya kusukuma mshambulizi kwani mbali ya kuwa na uwezo wa kuzuia mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa ni mzuri kwenye hilo.
Kikosi cha Simba kilichoanza: Lakred, Kapombe, Mohammed Hussein, Che Malone, Inonga, Sarr, Ngoma, Chama, Kibu, Jobe na Saido.